.

.
Tuesday, January 8, 2013

9:26 PM
WATU sita wamefariki dunia na wengine zaidi ya 110 wamelazwa na kuruhusiwa kutokana na kuugua ugonjwa wa kipindukipindu katika Kata ya Muze wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Idadi hiyo inatokana na wagonjwa walioripoti kwenye kituo cha kipindupindu cha Kata ya Muze, ingawa kuna taarifa zinazoeleza kuwa wapo watu wengine ambao wameugua na kufa katika kambi za wavuvi za ng’ambo ya Ziwa Rukwa na kufa kimyakimya pasipo serikali kuarifiwa.
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa ugonjwa huo umelipuka kwa muda mrefu katika bonde la Ziwa Rukwa lakini umekuwa ukipungua na kurejea tena na kuongezeka kasi yake katika kipindi cha mwezi Desemba mwaka jana baada ya kambi ya wavuvi ya Kijiji cha Ilanga kukumbwa na tatizo hilo.
Hata hivyo tatizo hilo limeonekana kuongezeka katika kipindi hiki cha mvua kutokana na maeneo mengi katika bonde hilo la Ziwa Rukwa wakazi wake kutokuwa na vyoo huku baadhi ya maofisa wa afya wakituhumiwa kuchangia tatizo hilo kwa kueendekeza vitendo vya rushwa katika misako wanayoifanya kuwabaini wale wasio na vyoo.
“Zoezi la ujenzi wa vyoo kwenye maeneo ya kambi za wavuvi na vijiji jirani limekuwa gumu kwani kuna watu wamekuwa wakithubutu hata kuwapiga maofisa afya wanaokwenda kufanya ukaguzi kwenye maeneo hayo ya kambi za wavuvi na mwisho wa siku wanaishia kumalizana kinyemela kwa kulipana fedha huku bado tatizo la kipindupindu likiendelea,” alisema mmoja wa wakazi wa Muze ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Kutokana na hali hiyo juzi, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang’a, alifanya ziara ya kushtukiza kwenye kambi ya kipindupindu ya Muze na kukuta wagonjwa wawili ambao wamelazwa kwenye kituo hicho wakiwa na hali mbaya, kutokana na uchafu na wagonjwa hao kukosa huduma muhimu huku mkuu wa wilaya hiyo akigeuka mbogo kwa watoa huduma na kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya.
Mmoja wa wagonjwa hao alikuwa amelazwa chini ya mti na kutundikiwa maji huku mwingine alikuwa amelazwa sakafuni ndani ya chumba kimoja kichafu na akiwa hajapatiwa huduma yoyote baada ya kituo hicho kukosa dawa hata maji ya kuwatundikia wagonjwa hao, hivyo kulazimika kununua wao wenyewe.
Kitendo hicho kilimkasirisha mkuu huyo wa wilaya na kulazimika kupiga simu kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Dk. Elina Yesaya akimtaka kueleza ni mkakati upi waliouchukua katika kudhibiti kipindupindu kwa muda wote huo.
Chang’a alielezea kusikitishwa kwake na taarifa zilizotolewa wiki iliyopita kwenye kikao cha Ulinzi na Usalama cha wilaya ambapo ofisi ya Mganga Mkuu alidai kuwa tatizo hilo limekwisha na hatua zimechukuliwa katika kuboresha kituo cha kipindupindu cha Muze ambacho Mkuu huyo wa wilaya alikikuta kikiwa kichafu na huku wahudumu wake wakikosa vifaa muhimu kama maji ya kutundikia wagonjwa na hata mipira ya kuvaa mikononi.
“Mganga kwanini unatesa hawa Watanzania, maana hapa nashuhudia wagonjwa wamejisaidia na hawajasafishwa, wamelazwa nje na mwingine kalazwa sakafuni, kituo kichafu na wewe upo! Hebu fikiria huyo angelikuwa mzazi wako halafu yupo kwenye hali hii ungejisikiaje? Na umekaa ofisini pasipo kufika kuona tatizo, nakuagiza ndani ya saa sita uwe umeshafika hapa na huduma bora imepatikana, wala usinichokoze zaidi,” alisema Chang’a wakati akizungumza na simu na Kaimu Mganga Mkuu.
Kwa upande wake Dk. Yesaya alisema wamekuwa wakipeleka huduma zote kwenye kambi hiyo na wagonjwa wanahudumiwa vizuri na hatua zimechukuliwa kudhibiti kipindupindu kinyume cha hali iliyokutwa na mkuu wa wilaya.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Kwela Ignas Malocha aliyekuwa ameongozana na Mkuu wa wilaya kutembelea kituo hicho alilazimika kutoa fedha zake na kwenda kununua maji ya kutundikia wagonjwa hao baada ya kulazwa kwa muda mrefu kwenye kituo hicho wakiwa wamekosa huduma kutokana na kukosa pesa za kununua maji ya kuwatundikia.
Wakati huo huo Chang’a aliagiza kufungwa kwa muda wa wiki mbili migahawa yote kwenye mji nwa Muze huku akiagiza uongozi wa kata hiyo kufanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba na migahawa hiyo ili kubaini zile ambazo hazina vyoo na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

0 comments:

Post a Comment