.

.
Sunday, January 27, 2013

10:03 PM
MKUU wa Wilaya ya Arusha, John Mongela ametoa kauli ya serikali kuwa Sekondari ya Korona haijafungwa kama ilivyotangazwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuwa mazingira yake hayawezi kutoa elimu bora.
Mongela alisema Lema hana nguvu ya kisheria kufunga shule, lakini akaahidi kushirikiana naye kushughulikia changamoto zinazoikabili kama ambavyo wamekuwa wakishirikiana.
“Naamini mbunge ana nia njema, ila kwenye hili suala la kufunga shule amepotoka kidogo, najua ni kiongozi aliyechanguliwa na wananchi wengi kutokana na busara zake kutetea haki ila alipaswa atumie njia sahihi kurekebisha makosa ya utendaji,” alisema Mongela.
Hata hivyo, Mongela alimsimamsha kazi Mkuu wa shule hiyo, John Mbise kutokana na kushindwa kutimiza wajibu, ikiwamo kwenda masomoni bila kibali cha mwajiri wake.
Alisema sheria namba 25 ya mwaka 1978, iliyofanyiwa mabadiliko katika sheria namba 10 mwaka 1998, inatamka wazi wanaohusika kufunga shule ni kamishna wa elimu, ofisa elimu mkoa, wilaya na viongozi wanaosimamia ulinzi na usalama ngazi ya mkoa na wilaya.
“Nchi yetu haiko kwenye vita na kuna mamlaka husika ambazo baada ya kujiridhisha zinaweza kuchukua hatua za kufunga shule, lakini sivyo alivyofanya mbunge ambaye ni mkazi wa Kata ya Engutoto na ameshiriki kikamilifu wakati wa kuanzishwa kwake,” alisema.
Alisema wabunge ndiyo watunga sheria. inashangaza kuona mbunge anakiuka misingi ya sheria kwa kuchukua uamuzi kinyume na taratibu za uongozi.
Mongela alimwagiza Ofisa Elimu Sekondari wa Jiji la Arusha, Violet Mlowosa kuhakikisha Jumatatu wanafunzi wanafika shuleni bila kukosa na atakayekosa bila sababu za msingi, atachukuliwa hatua za kisheria.
Pia, alitaka huduma ya maji kurejeshwa mara moja na deni wanalodaiwa kulipwa kwa Mamlaka ya Maji Arusha (Auwsa).
Alisisitiza suala hilo kutofanywa kisiasa kutokana na umuhimu wake kwa jamii na kumtaka ofisa elimu kupeleka majina ya watu waliopendekezwa kuunda bodi ya shule hiyo.
Madhumuni ya kujengwa shule hiyo yalikuwa iwe ya kidato cha tano na sita, lakini hamashauri ya jiji ikabadili malengo hayo baada ya wanafunzi wengi waliofaulu darasa kukosa nafasi.
Changamoto inayoikabili shule hiyo ni umbali wa takriban kilometa 16 kutoka katikati ya jiji.

0 comments:

Post a Comment