.

.
Saturday, April 20, 2013

1:31 AM

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa jana limepokea radio za mkononi 16 ambazo zilitolewa na Kampuni ya Emags Video Entertainments iliyopo jijini hapa. Akitoa radio hizo, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Elias Magesa alisema kwamba, wameamua kutoa radio hizo ili ziweze kurahisisha mawasiliano ndani ya jeshi hilo.

Bwana Magesa alisema radio hizo zenye thamani ya Tsh 2.6 Mil. zitaweza kulisaidia jeshi hilo kuimarisha ulinzi katika shughuli zake za kila siku. Alisema kupitia mawasiliano kutawezesha askari kuwasiliana na hatimaye kufanikisha kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu.

“Suala la Ulinzi si la jeshi la Polisi pekee bali ni la watu wote ndio maana kwa kutambua hilo Kampuni yetu ya EMAGS Video Entertainments imeaua kutoa radio hizo kwa jeshi hilo kwani kwa kufanya hivyo naona tutakuwa tumeshiriki kwa namna moja au nyingine katika dhana ya ulinzi shirikishi”. Alifafanua Bw. Magesa.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahimu Kilongo akipokea radio hizo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alitoa shukrani zake kwa kampuni hiyo na kuongeza kwamba, amefarijika sana na moyo ulioonyeshwa na Bw. Elias Magesa pamoja na kampuni yake kwani si wote wanaoweza kufanya hivyo.

“Kutoa ni moyo si lazima uwe na kitu kikubwa sana ndipo utoe unaweza kuwa na chochote na ukatoa kama kampuni hii ilivyofanya. “ Alisema Kaimu Kamanda huyo.

Alisema radio hizo zimepatikana muda muafaka kwani bado kuna changamoto ya upungufu wa vitendea kazi na kuongeza kwamba zitasaidia sana katika kuimarisha hali ya usalama kwani zitakuwa zinatumika na askari wa jeshi hilo katika doria na maeneo mbalimbali hali ambayo itasaidia kuimarisha mawasiliano.

Kaimu Kamanda Kilongo alitoa wito kwa wadau wengine wa mkoa huu kuiga mfano wa Kampuni hiyo kwa kujitokeza kuchangia vitendea kazi vitakavyosaidia kurahisisha utendaji ndani ya jeshi hilo.

Naye Afisa Uhusiano wa Kampuni hiyo Bw. Severinus Mwijage alisema pamoja na kujishughulisha na utengenezaji wa filamu lakini pia wameona wawe karibu na Jamii ambao ni wadau wao wakubwa kwa kutoa radio hizo ambazo zitasaidia mawasiliano ya ndani ya jeshi la polisi na hatimaye kuimarisha ulinzi katika maeneo ya wananchi hao.

0 comments:

Post a Comment