.

.
Tuesday, April 16, 2013

2:59 AM
Waandishi wa habari wametakiwa kujikita zaidi kwenye habari za kiuchunguzi na utafiti (makala) kuliko habari za matukio pekee hali itakayowasaidia kupata mafanikio makubwa kwenye fani na katika maisha yao sanjari na kujenga heshima katika jamii.
 
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi wa Jambo Arusha Publisher ambae pia ni mmiliki wa gazeti la Kutoka Arusha Anjelo Mwoleka alipokuwa Akihutubia kwenye mahafali ya chuo cha Uandishi wa habari na utangazaji Arusha (AJTC) yalifanyika hivi karibuni kwa Mrombo iliyoko wilaya ya Arusha mkoani hapa.
 
Mwoleka ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo alisema kuwa Waandishi wengi wa sasa wanashindwa kuendelea kifani na kimaisha na wengine hata kudharaulika na jamii kwa kupenda kuandika habari za matukio hasa za kipolisi au za mikutano hali ambayo inashusha hadhi ya taaluma ya Uandishi wa habari hivyo kila mwandishi apende zaidi kuandika habari za kiutafiti,
 
“Waandishi wengi utakuta kazi yao kubwa ni kuandika tu habari za matukio na mikutani kuwa kamanda wa mahala Fulani amesema wa mkoa huu amesema……..na sasa imefikia hadi sasa wanaandaliwa taarifa (press) kwa kujulikana kuwa hawapendi kujishughulisha, hivyo niwaombe tu kuwa hali isiendekezwe kama kweli wewe ni mtu unayependa kuendelea kifani na maisha kwa ujumla badala yake andaeni vipindi vya redio na televisheni au kuandika makala kwenye magazeti kwani itakusaidia kujua mambo mengi na kukupa heshima kama mwandishi mzuri” alisema Mwoleka.
 
Mbali na hilo pia amewataka waaandishi wasiwe na ukomo wa elimu bali wawe na hamu ya kujiendeleza zaidi ikiwemo masoma ya kujikita katika habari za aina moja, pia wawe waadilifu kimaadili na mavazi ili kuweza kurahisisha kupata habari kwenye vyanzo vya habari au wadau sanjari na kutokutegemea kuajiriwa zaidi kuliko kujiajiri,
 
“Niwaombe tu leo mnapomaliza elimu yenu mkiingia kazini mkawe waadilifu kwa kuvaa mavazi ya heshima pia mnapoenda kwa wadau msiwe wa kwanza wa kuwatishia wadau kuwapa pesa ili msiwaandike vibaya kwani huo ni wizi kama wizi mwingine hali itayopelekea kupigwa, kutekwa au hata kuteswa kwa tabia zisizo za kimaadili” aliongeza Mwoleka.
 
Mwoleka pia aliwataka wahitimu hao kufuata vigezo tisa za mwandishi bora kuwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya lugha, kuwa na uhakika wa habari wanazoziandika, kuwa vyanzo vingi vya habari pia kufanya utafiti wa kutosha juu ya habari watazozinadika, kuzingatia usahihi wa habari, pia kuwa makini katika matumizi ya takwim sanjari na uwiano wa habari wanazoziandika.
 
Awali katika risala iliyosomwa na wanafunzi hao walisema kuwa katika chuo hicho wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo jengo maktaba, vifaa vya kusoma kwa vitendo kama kamera za picha za kawaida, video na mike za kutosha.
 
akimkaribisha mgeni rasmi mkurugenzi wa chuo hicho cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha( AJTC) Joseph Mayagila alisema wanafunzi wanaohitimu kwa siku hiyo ni wanafunzi 52 kwa ngazi tofauti ikiwemo ngazi ya cheti na stashahada ya uandishi wa habari na utangazaji.

0 comments:

Post a Comment