.

.
Wednesday, April 3, 2013

Baadhi ya viongozi wa uamsho wakipelekwa mahakamani.  

ZANZIBAR.
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mwanakwerekwe imeifuta kesi moja inayowakabili viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), kutokana na kuchukua muda mrefu bila ushahidi wake kukamilika.

Hakimu Ame Msaraka Pinja alisema jana kuwa, anaifuta kesi hiyo kwa kutumia kifungu cha 209 cha makosa ya jinai.

Washtakiwa wa kesi hiyo ambayo ilikuwa ni moja kati ya tatu zinazowakabili ikiwa kwenye Mahakama hiyo na nyingine Mahakama Kuu, walikuwa wanakabiliwa na kesi ya kuhatarisha amani kwa kutoa lugha kali.

Ilipotajwa mara ya mwisho, Machi 19 mwaka huu upande wa mashtaka ulidai kuwa, upelelezi  haujakamilika na mawakili wa utetezi walimwomba hakimu kuifuta kwa vile washtakiwa wako ndani muda mrefu.

Wakili wa washtakiwa hao, Salum Toufik na Abdallah Juma walimwomba hakimu kutokana na taratibu za Mahakama hususan makosa ya jinai, kesi inapofikia  miezi mitatu na kuendelea bila  upelelezi kukamilika inapaswa kufutwa.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Khamis Jafar waliomba Mahakama kuwapa muda zaidi kutokana na kuchukua kipindi kirefu bila upelelezi kukamilika.

Washtakiwa hao ni Masheikh Farid Hadi, Mselem Ali, Mussa Juma, Azza Khalid Hamdan, Suleiman Juma, Khamis Ali na Hassan Bakari. 

Washtakiwa hao bado wanakabiliwa na kesi iliyopo chini ya Hakimu wa Wilaya, Khamis Rashid na washtakiwa wanne wapo nje kwa dhamana, huku watatu wakiwa rumande kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.  

Washtakiwa watatu ambao walikwenda katika kesi hiyo wakitokea rumande ni Masheikh Farid, Juma Suleiman na Mussa Juma.

0 comments:

Post a Comment