.

.
Wednesday, April 3, 2013

 

Dar es Salaam. 
 Mamlaka ya Udhibiti wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imepandisha nauli za daladala, mabasi ya kwenda mikoani, usafiri wa reli na tozo za majini kuanzia Aprili 12, mwaka huu.Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Ahmad Kilima alisema jana kuwa nauli za daladala zimeongezeka kwa asilimia 24.46 kwa kuzingatia maoni ya wadau na gharama za uendeshaji.


Kwa upande wa usafiri wa daladala nauli zimepanda kwa umbali tofauti kutoka Sh300 hadi 400, Sh350 hadi 450, Sh500 hadi 600, Sh650 – 750 na kwa wanafunzi kutoka Sh150 hadi 200 katika sehemu yoyote watakayokwenda.


Nauli za usafiri wa mabasi makubwa ya masafa marefu nauli hizo zimeongezeka kwa viwango tofauti. Mathalan kwa basi la kawaida kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ni Sh30,700, njia ya vumbi kutoka Kigoma hadi Sumbawanga Sh25,400 na basi la hadhi ya kati (Semi Luxury) kati ya Dar na Mwanza ni Sh61,400, wakati basi la hadhi ya juu (Luxury) kati ya Dar na Arusha ni Sh 36,000.


Kilima alisema: “Kuanzia Aprili 12 mwaka huu, kati ya kilometa 0 hadi 10, nauli ya daladala itakuwa Sh400 badala ya Sh300 zinazolipwa hivi sasa.
“Pia nauli za mabasi ya kwenda mikoani zimeongezeka kwa asilimia 20.3 kwa mabasi ya kawaida, mabasi ya kati kwa asilimia 16.9 na mabasi ya daraja la juu kwa asilimia 13.2,” alisema.


Kilima alisema nauli za mabasi ya mikoani zimepanda kutoka Sh30.67 hadi Sh36.89 kwa kilometa kwa mabasi ya daraja la kawaida katika njia za lami.
Kwa upande wa mabasi ya kawaida kwa njia ya vumbi imepanda kutoka Sh37.72 hadi Sh 46.11 kwa kilometa na kwamba mabasi ya hadhi ya kati, nauli zimepanda kutoka Sh45.53 hadi Sh 53.22 kwa kilometa.

0 comments:

Post a Comment