.

.
Wednesday, April 3, 2013

10:41 PM
MKAGUZI KATIKA MACHINJIO YA MKOA WA MOROGORO DK PUPA JOSEPH AKIKAGUA NYAMA YA NG'OMBE KABLA YA KWENDA KUUZWA KATIKA MABUCHA HIVI KARIBUNI.

TUNDUMA. 
VURUGU kubwa zilizuka jana katika Mji wa Tunduma ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, baada kutokea mvutano mkali kuhusu nani anayepaswa kuchinja mifugo baina ya waumini wa dini mbili; Waislamu na Wakristo.

Mamia ya polisi kutoka wilaya zinazouzunguka Mji wa Tunduma walimwagwa na walilazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji pia, kutuliza vurugu zilizodumu kwa zaidi ya saa nne.
Vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani, zimetokea siku tatu tu tangu Rais Jakaya Kikwete aonye kwamba kwamba vurugu zenye sura ya kidini ni hatari na zinaweza kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi nchini.

Mijadala kuhusu vurugu hizo ilitawala katika mitandao ya kijamii ikiwamo facebook, Mabadiliko Forum na Jamii Forums ambako watu mbalimbali walionyesha kukerwa nazo, huku wakiitaka Serikali ichukue hatua za kudhibiti.

Kutokana na vurugu hizo zilizoanza saa 4:30 asubuhi, wakazi wa mji huo walijifungia ndani kwa kuhofia usalama wa maisha yao, huku maduka na shughuli za biashara nazo zikifungwa.


Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba katika vurugu hizo, watu zaidi ya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.

Habari zaidi zinasema barabara za mji huo zilifungwa, umeme ulizimika baada ya moto kulipuka kwenye moja ya nguzo za umeme. Pia mpaka wa Tanzania na Zambia ulifungwa kwa muda.

Magari ya abiria na yale ya usafirishaji yaliyokuwa yakitoka na kuelekea Zambia, Dar es Salaam, Sumbawanga na Mbeya Mjini pia yalikwama na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria. Msikiti ulivunjwa na watu wawili akiwamo askari polisi walijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wahusika katika mgogoro wakiwamo viongozi wa dini na wachinjaji wa nyama.

“Mgogoro wa kuchinja umedumu kwa siku tatu, jana kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ilikutana na baadhi ya viongozi wa dini na wadau wa kuchinja nyama na kuna mambo matatu ambayo yalitolewa katika mkutano huo,” alisema Diwani.

Alisema katika mkutano huo Kandoro aliagiza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki, ambacho Serikali ngazi ya kitaifa inalishughulikia na kuwataka kuendelea na hali uchinjaji kama ilivyokuwa awali na kila mmoja afanye kile anachoamini katika dini yake wakati wa kula.

Hata hivyo, baadhi ya Wakristo waliafikia lakini wengine hawakuafiki. Hivyo jana asubuhi walihamasisha maandamano katika mji huo ambayo yalisababisha vurugu hizo.

“Pamoja na hayo yote uchunguzi wa kitaalamu tumebaini kuwa vurugu hizo siyo za kidini, bali zimehusishwa siasa kwani hata viongozi wa dini waliohusika ni baadhi siyo wote ambao wanajishughulisha na suala hili,” alisema Diwani.

chanzo :   http://www.mwananchi.co.tz

0 comments:

Post a Comment