.

.
Monday, April 15, 2013

12:16 PM
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limesema litaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kulinda na kutetea haki za watoto. Hayo yalisemwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mary Lugola ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa mtaani duniani.
Katika maadhimisho hayo ambayo yalifanyika tarehe 12 mwezi huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa, Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi alisema kwamba jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na watoto mkoani hapa limekuwa karibu sana kiutendaji na mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya serikali kama vile Mkombozi, CCR, Action For Children n.k katika kutetea na kulinda haki za watoto wa mitaani.
Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha alisema mbali na jeshi hilo kujihusisha katika kutetea na kulinda haki za watoto wa jamii hiyo, pia linasaidia kuinua na kuibua vipaji vya watoto hao kupitia programu ya MWONGORIKA ya Polisi jamii ambayo inajihusisha na michezo kwa vijana.
Alisema kupitia Dawati hilo, jeshi la polisi limeweza kuwahudumia watoto wa mitaani kwa kushirikiana na mashirika hayo ili kuwawezesha waishi katika mazingira salama na kupata mahitaji muhimu.
 “Kwa mfano tumeshawahi kuwaunganisha na wazazi wao pamoja na kuwasafirisha kwenda makwao watoto waliokuwa tayari kurudi ”. Alisema Bi. Lugola.
Alimalizia kwa kusema kwamba Dawati la Jinsia na watoto huwa linahakikisha linapata taarifa za watoto walioathirika na pia wale wote wanaowanyanyasa watoto hao wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Nalo shirika la Mkombozi kupitia risala yao iliyosomwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Shirika hilo Bi. Doris Cornell alisema kwamba ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku hiyo ni “Nyumbani Mtaani Nyumbani” ikiwa na maana ya kwamba, mtoto atatoka nyumbani kwenda mtaani na kisha atarudi nyumbani.
Alisema lengo la siku hiyo ni kuwapa jukwaa watoto waishio na kufanya kazi mtaani wakiungana na wengine duniani kote kupaza sauti ili haki zao zisiipuzwe.
Bi. Doris alisema watoto waishio mitaani na kulala mitaani wanazofursa na haki sawa na watoto wengine duniani na kwamba wana haki ya kuishi, kulindwa, kuendelea na kushiriki katika mambo yanayogusa maisha yao kama ilivyoainishwa katika mkataba wa Kimataifa wa haki za watoto kifungu cha 4.
Risala hiyo ilieleza sababu za kuwepo kwa watoto hao mitaani ni pamoja na kukosa haki za msingi (chakula, malazi, mavazi, ulinzi, elimu, upendo, matibabu n.k) kutoka katika familia zao, kufiwa na mzazi mmoja au wote wawili,
Sababu nyingine ni vitendo vya unyanyasaji na ukatili waliofanyiwa katika jamii au familia, kipato duni katika familia/wazazi/walezi, utumikishwaji wa watoto (ajira za watoto), kubaguliwa na kunyang’anywa mali za wazazi wao.
Siku hiyo ambayo huwa inaadhimishwa katika nchi 130 duniani, Tanzania na Uingereza ikiwa ni miongoni mwa nchi hizo, ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya pamoja na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Maria Maswa.
 

0 comments:

Post a Comment