.

.
Friday, April 5, 2013

Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe (wapili kutoka kulia) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu tamko la Serikali juu ya mgogoro wa mpaka wa ziwa Nyasa. (wa kwanza kulia) ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo John Haule.
 
SERIKALI ya Tanzania imeomba  Malawi iache kutapatapa kuhusu mgogoro wa mipaka wa ziwa Nyasa kufuatia Rais  wa nchi hiyo, Joyce Banda kutangaza katika  baadhi ya vyombo vya  habari  kuwa atapeleka  suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ), badala yake isubiri uamuzi wa jopo la usuluhishi lifanye kazi na litoe maamuzi.
 
Aidha serikali  imesema kuwa hata siku moja  haijapelekewa taarifa wala nyaraka za siri kutoka kwa Katibu wa jopo hilo, ambalo linahusisha marais wastaafu wa zamani wa Afrika na wanasheria  kama ilivyodaiwa  na  Rais  Banda katika vyombo hivyo , kuwa kuna Mtanzania anayeitwa Dk. John Tesha ambaye wanaamini ametoa  habari na kuiba nyaraka za siri.
 
Akilitolea ufafanuzi   jambo hili, Waziri Membe amesema kuwa  Tanzania na jopo hilo   limestushwa juu ya madai hayo na hatua ya Rais Banda kupoteza imani.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard  Membe, wakati akizungumzia na waandishi wa habari juu ya mgogoro huu  kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara jijini Dar es Salaam. 
 
Kwa kuwa baada ya kuwasilisha barua na nyaraka zake Dk. Tesha hatahusika katika suala hilo ili kuondoa uwezekano wa nchi  hiyo (wenzetu)  kulalamika. Pia   hata marais wastaaafu kutoka katika nchi zenye migogoro ya mipaka   hawatahusika  kwa sababu ya  kuzuia ‘confilict of interest’.   
 
“ Serikali ya Tanzania ina imani  na jopo linaloongizwa na Rais mstaafu wa Msumbiji , Joachim Chissano na marais wengine ambao ni  Festus Mogae na Thabo Mbeki ,  kwa kuwa lina watu wenye uzoefu, wataalamu na wachapakazi.  Pia kuna jopo la   wanasheria   na wataalamu wa masuala ya   migogoro limeundwa na ni la watu saba,”alisisitiza Waziri Membe.
 
Aliwataja  wanasheria hao kuwa ni Jaji Raymond Ranjeva, ambaye ni Jaji mstaafu wa ICJ, Profesa George Kanyeihamba(Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Uganda, Jaji Baney Afako (Mshauri wa masuala ya sheria kwenye Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan), Dk. Gbanga Oduntun(Profesa  wa  Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa mpaka kati ya Nigeria na Cameroon).
 
Wengine ni Profesa Martin   Pratt, (ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Geografia na Mipaka), Dk. Dire David Tladi (Mjumbe wa Kamisheni  ya Sheria ya Umoja wa Mataifa) na Miguel Chisano(Kiongozi wa Chuo kinachoshughulikia mipaka ya Baharini na Nchi Kavu. 
 
“Ni watu wenye heshima ya dunia tusingetegemea--- kusema hana imani na jopo hili,” alisema.
 
Akirejea mazungumzo ya makubaliano yaliyofanyika Novemba 17, mwaka jana(2012) kuwa walikubaliana  hapo walipo katika jopo hilo ndipo sehemu ya mwisho. Hivyo wataenda ICJ iwapo watashauriwa na jopo la mzee Chissano.
 
‘’Wakati   tunasubiri jopo kufanya kazi na kutoa majibu serikali inaiomba Malawi pale katikati ya Ziwa Nyasa pasiguswe mpaka jibu litakapotolewa na jopo la usuluhishi. 
 
Tunaiomba serikali ya Malawi irudi katika jopo la usuluhishi na tutashangaa  ikiwa Malawi itakwenda  kushtaki ICJ   kwa kuwa  ili Malawi iende ICJ ni lazima sisi  tukubali. Hata pale tutakaposhauriwa   ni lazima sisi tukubaliane na Malawi,” alisisitiza  Waziri Membe.
 
Hivyo aliiomba  serikali ya  Malawi iache kutapatapa mara Uingereza, Marekani ,Jumuia ya Madola na Umoja wa Afrika(AU) na kuona viongozi mbalimbali wa dunia, bali iamini jopo la Mzee Chissano. Matokeo ya utafiti wao  upo uwezekano wa kuyakubali au kuyakataa. 
 
Akizungumzia kuhusu utoaji wa ripoti ya jopo hilo utakuwa ni lini,Waziri Membe alisema Tanzania haina haraka juu ya jambo hilo.
 
Waziri Membe  alisema  Tanzania , ilipeleka wataalamu Uingereza na Ujerumani ili kupata uelewa wa kutosha  juu ya jambo hilo, hivyo ina ushahidi wa kutosha.
 

0 comments:

Post a Comment