.

.
Saturday, May 25, 2013

2:19 AM
 
KATIBU MKUU WA CCM, ABDULRAHMAN KINANA.
KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kwa mara nyingine imezidi kumbana Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ikimtaka mwendesha mashitaka wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kumfungulia mashitaka ya kutorosha pembe za ndovu katika mahakama ya Afrika Mashariki.

http://polis.parliament.go.tz/images/Pictures/1608.jpgRaya Ibrahim Khamis.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo jana kwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2013/2014, Raya Ibrahim Khamis kwa niaba ya msemaji mkuu Ezekiel Wenje, alitaka Tanzania iombe msaada wa Kenya yenye ubalozi wa Vietnam ili kurahisisha upatikanaji wa ushahidi badala ya kutegemea ubalozi wake ulioko China.

Raya alisema madhumuni ya kumfungulia kesi Kinana yana lengo la kuudhibiti mtandao wa majangili na wafanyabiashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa wanataka Kina
na afunguliwe kesi kutokana na meli anazosimamia mojawapo ilikamatwa na shehena za pembe za ndovu huko Vietnam mwaka 2009.

Hii ni mara ya pili kwa kambi hiyo kuibua tuhuma hizo dhidi ya Kinana ambapo kwa mara ya kwanza msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alihoji jambo hilo na kupata upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM.

Raya alisema kuwa biashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika Mashariki inakua kwa kasi jambo linalotishia kutoweka kwa wanyama ndovu ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.

Alisema kuwa taarifa katika mtandao wa habari wa “Annamiticus” (www.annamiticus.com) zinasema kwamba mwaka jana, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania yalikamatwa huko Hong Kong yakiwa yamebeba tani 4 (kilo 4,000) za pembe za ndovu.

“Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa limeandikwa “plastic scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki, lakini baada ya kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa.

“Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za ndovu sawa na kilogramu 1,884,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa hiyo, wingi wa pembe hizo za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo 600 kwa uchache waliuawa.

Aliongeza kuwa mwezi uliopita kontena jingine limekamatwa limesheheni pembe za ndovu 113 huko China zenye thamani ya dola za Marekani 400,000 likiwa limeandikwa kwamba limebeba vipuri (spareparts) kutoka Burundi.

“Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo waliouawa Tanzania,” aliongeza.

Alisema kambi hiyo inataka kujua kama Serikali ya Tanzania imefanya mawasiliano na Burundi ili kujua ukweli kuhusu kontena lililosheheni pembe za ndovu lililokamatwa huko China.

Aliongeza kuwa kwa kuzingatia utekelezaji wa mpango mkakati wa amani na usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kubadilishana taarifa za uhalifu na usalama, ni vema serikali ikiwasiliana na wote wanaoweza kukamilisha uchunguzi husika.

Alisema kuwa kuna Watanzania walioshutumiwa na kusutwa kuhusika na mtandao huu wa biashara hii haramu ya pembe za ndovu akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Kinana.

“Kwa kuwa Serikali ya Tanzania inaonekana dhahiri kumtetea na kumlinda mtu huyu kwa kuwa ni kiongozi mkubwa wa chama tawala, kama alivyofanya Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi alipokuwa anatoa mchango wake kwenye bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Aprili 30 mwaka huu.

“Na kwa kuwa tembo wengi wa Afrika Mashariki wanazidi kupotea kila siku kutokana na biashara hii haramu ya pembe za ndovu, jambo ambalo linaikosesha Jumuiya ya Afrika Mashariki mapato yatokanayo na utalii na hivyo kuiweka hatarini sekta ya utalii ya Afrika Mashariki, watu hawa lazima washtakiwe,” alisema.

Raya pia aligusia uhuru wa habari kwa nchi wanachama huku akinukuu taarifa ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ya Mei 20 mwaka huu ambayo ilisema kuwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameamuru kufungiwa kwa gazeti la kila siku la nchi hiyo la “The Daily Monitor”, na gazeti lingine la “Red Pepper”.

Hatua hiyo ni kutokana na kuchapisha habari iliyofichua njama za Rais Museveni za kumuandaa mtoto wake, Muhoozi Kainerugaba ambaye ni brigedia wa jeshi kuwa rais wa nchi hiyo baada ya yeye kuondoka madarakani.

Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliomba mwongozo wa kiti akitaka wapinzani wakemewe kwa kukiuka kanuni na kutaja majina ya viongozi wakuu wa nchi kwa dhihaka.

“Mimi sitaki kuzungumzia suala la Kinana maana hizo ni porojo wacha waendelee, lakini nazungumzia ukiukwaji wa makusudi wa kanuni na kumtaja Rais Museveni kwa mambo ambayo eti msemaji ameyasikia kwenye redio pamoja na lile la Kinana japo tumeishajibu, lakini wanaendelea kujifurahisha. Naomba ukemee jambo hili,” alisema.

Hata hivyo, baada ya Lukuvi kuketi, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika naye aliomba mwongozo akitumia kanuni inayomruhusu mbunge kunukuu taarifa kwenye vyombo vya habari akisema kuwa Raya alikuwa sahihi.

Sitta amkingia kifua
Akijibu hoja hiyo wakati wa majumuisho, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliwataka CHADEMA wamuache Kinana afanye siasa na majibu watayaona mwaka 2015.

Sitta alisema CHADEMA imekuwa ikitumia nguvu kulazimisha hoja zao na inaonekana Kinana ndiye anayewakera kwa kuwa hatoki midomoni mwao.

“Kila siku Kinana…Kinana…jamani hebu acheni kumhusisha na biashara haramu ya pembe za ndovu,” alisema.

0 comments:

Post a Comment