TTHE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) kimesikitishwa
sana na vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei 2013 na uvunjaji mkubwa
wa haki za binadamu uliofanywa na polisi tarehe 23 Mei 2013.
Chimbuko la
mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali
ya CCM kutekeleza ahadi zaka za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na
Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua ume
me wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa.
me wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa.
CUF inalaani vikali vitendo vya kihalifu vya kuchomea nyumba ya
mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim
Mikongolo, na nyumba za baadhi ya viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani
vikali vitendo vya kuhujumu miundombinu muhimu likiwemo daraja la
Mikindani linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es
Salaam.
CUF imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya askari wanne wa JWTZ
kwa ajali ya gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao wakisafirishwa
toka Nachingwea kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti vurugu.
Tumepeleka
salamu za pole kwa CDF Jenerali Mwamunyange na kupitia kwake kwa familia
za marehemu.
Tunawapa pole askari wote waliojeruhiwa na kuwaombea kwa
Mwenyezi Mungu wapone haraka na waweze kurejea katika ulinzi wa taifa
letu.
Vilevile tumesikitishwa na kifo cha raia wawili kwa kupigwa risasi
akiwemo mama mjamzito na raia wengi kujeruhiwa. Tunawapa pole familia za
marehemu na kuwaombea wote waloumia wapone haraka na waendelee na
shughuli zao.
Taarifa za vyombo vya habari vinaeleza kuwa ghasia hizi zilianza
baada ya hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini iliyosomwa
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza ujenzi wa
bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Taarifa tulizozipata toka Mtwara zinaeleza kuwa jana kuanzia
asubuhi, wakati Waziri Nchimbi akisoma tamko la serikali bungeni kwa
niaba ya Waziri Mkuu kuwa hali ya Mtwara sasa ni shwari askari wa Jeshi
la Polisi walifanya vitendo vya kinyama kwa raia wasio na hatia.
Polisi
walipita katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana, kuwapiga na
kuwachukua kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi za
moto zilipigwa hovyo hovyo.
Aidha katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo
waliwapiga wake zao, watoto wadogo na hata wazee kwa madai kwamba
vijana wao wanasumbua. Binti mjamzito aitwae Fatuma alipigwa risasi na
kufariki.
Katika eneo la Mkana Read, Polisi walichoma moto soko la
wananchi, nyumba nyingi za raia zimechomwa moto na polisi wamepora mali
za watu zikiwemo za maduka ya wafanyabiashara.
Wananchi wengi wakiwemo
wanawake wamelazimika kukimbia nyumba zao. Taarifa tulizopata zinaeleza
vitendo vya kinyama vya polisi vilisita baada ya maafisa wa juu wa Jeshi
la Polisi kufika Mtwara.
Vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei hazihalalishi Jeshi la
Polisi kupiga watu, kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda vya biashara na
kupora mali za watu wasio na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora mali
na kuchoma vibanda vilitokea Tandahimba mwaka jana. Weledi ndani ya
Jeshi la Polisi uko chini sana.
Tunalaani vikali vitendo vya Jeshi la
Polisi la kupiga watu, kuchoma nyumba na kupora. Uongozi wa Jeshi la
Polisi uchukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya polisi
waliohusika na vitendo hivyo.
Tunatoa wito kwa asasi za haki za binadamu
na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia wahanga wa Mtwara kudai haki
zao.
Pamoja na kulaani vitendo hivi vya kihalifu na kuchukua hatua za
kisheria dhidi ya wale waliohusika na vitendo hivyo, Serikali itafanya
makosa makubwa na kuingiza nchi katika mgogoro wa muda mrefu na wananchi
wa mikoa ya kusini ikiwa itafumbia macho chimbuko la mgogoro huu na
kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni matokeo ya uchochezi wa
wanasiasa wachache wanaojitafutia umaarufu.
Narudia Chimbuko la mgogoro
wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM
kutekeleza ahadi za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay
mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na
kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa.
Mradi
mwingine ni kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi kama
malighafi kama ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki
visima vya gesi ya Mnazi Bay na Msimbati.
Kama miradi hii ingeanza
kutekelezwa nina uhakika wananchi wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga
gesi ya ziada kusafirishwa Dar es Salaam.
Kauli ya Waziri Nchimbi Bungeni kuwa serikali itawasaka waasisi wa
vurugu hizi ndani na nje ya Mtwara ni juhudi za kutafuta mchawi badala
ya kutathmini kwa nini wananchi wa Mtwara hawaiamini kabisa serikali ya
CCM.
Tumepata taarifa kuwa pana mpango kabambe wa kuwakamata viongozi
mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa wanaohusika na kuchochea,
kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na wafuasi wa CUF.
Serikali ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito watu wasiokuwa na
hatia. CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la gesi
tumejenga hoja za kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu
utekelezaji wa miradi ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza.
Viongozi wa CUF hawajachochea vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya
hadhara na maandamano ya amani kujenga hoja za kimsingi.
Mimi binafsi nilienda Mtwara mwaka jana nikazuwiwa kufanya mkutano
wa hadhara Mtwara mjini kwa madai kuwa hali siyo shwari wilaya ya
Tandahimba.
Wananchi wa Mtwara walitaka nifanye mkutano huo pamoja na
kuwa umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye hivyo na wakakubali.
Tarehe 14 Aprili 2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya mkutano wa
hadhara sikukaidi nikafanya mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu Mkuu
wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya
mkoa wa Mtwara akaambiwa hana ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara mkoa
wa Mtwara na hivyo akasitisha ziara yake.
Kuwakamata viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na Lindi na wa
kitaifa hakutamaliza mgogoro kati ya serikali na wananchi wa Mtwara
ikiwa serikali itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza. Badala
yake itaongeza chuki dhidi ya serikali.
Wakati wananchi wa Mtwara wamepoteza imani kwa uongozi wa CCM na
serikali yake, Serikali imezuia vyama vingine vya siasa na asasi za
kiraia kufanya shughuli za kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa hiyo
kuunyima umma miongozo ya kisiasa za demokrasia.
Umma uliokata tamaa na
unaoamini unabezwa, kudharauliwa na kudanganywa na watawala unaweza
kuchukua hatua zenye madhara hata kwa maslahi yao wenyewe.
Serikali imekuwa inapotosha kwa makusudi madai ya msingi ya
wananchi wa Mtwara ambayo ni kuwa serikali itekeleze miradi ya gesi
iliyoahidi wananchi wa Mtwara.
Badala yake wananchi wa mikoa mingine
wanalishwa sumu kuwa Wananchi wa Mtwara hawataki raslimali ya gesi
iwanufaishe Watanzania wengine.
Umeme ukifuliwa Mtwara na kuunganishwa
katika gridi ya taifa utatumiwa na wote waliounganishwa na gridi ya
taifa. Kiwanda cha mbolea cha Mtwara kitazalisha mbolea itakayotumiwa
nchi nzima. Wananchi wa Mtwara hawajasema Watanzania wengine hawana haki
ya kwenda Mtwara kupata ajira au kufanya shughuli za kibiashara.
Wanaobomoa umoja na mshikamano wa kitaifa ni wale wanaowabeza,
kuwadharau na kuendelea kuwadanganya wananchi wa Mtwara na kupandikiza
sumu kwa Watanzania wengine kwa kupotosha madai ya msingi ya wananchi wa
Mtwara na kushindwa kwa serikali kuwajibika kisiasa kwa ahadi ambazo
viongozi akiwemo Rais alizitoa kwa wananchi wa Mtwara.
Wananchi wa Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka sahihi na kupeleka
ombi (petition) kupitia Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni kujadili
kutekelezwa kwa miradi ya gesi ya Mtwara. Spika Anna Makinda kazuwia
ombi hilo kujadiliwa.
Bunge limeshindwa kuisimamia serikali na kuhoji kwa nini mradi wa
kufua umeme MW 300 ambao katika mwaka wa bajeti wa 2011/12 ulitengewa na
kutumia shilingi 540 milioni umesitishwa.
Mpaka hivi sasa hakuna kamati
ya Bunge iliyoenda kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala yake
Spika amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala
ya kuhakikisha kuwa Bunge linaisisimamia serikali.
Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri kaeleza serikali
kupitia TANESCO kwa kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion itajenga
kituo cha kufua umeme cha MW 400 na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa
kupitia Songea. Hata hivyo bajeti ya maendeleo haijautaja mradi huu
wala kutenga hata shilingi 1 kwenye mradi.
Wananchi wa Mtwara wanaona
wanaendelea kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo, majigambo na kauli
za kejeli za Waziri wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa wananchi wa Mtwara
katika masuala ya gesi zinazidi kuongeza chuki na jazba za wananchi.
Mpaka hivi sasa serikali imekataa kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa bomba
na upembuzi yakinifu wa mradi huu. Hotuba ya bajeti ya Waziri wa
Nishati haielezi kama Wentworth Resources wanaoendesha visima vya gesi
wataweza kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi
kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya kutumia
gesi mkoani Mtwara.
Linalonistusha na kunitisha ni kwa nini viongozi wa juu wa serikali
hawataki kuwa wawazi kuhusu mradi huu na wako tayari kupotosha,
kuwagawa wananchi na kudanganya alimuradi mradi huu utekelezwe na
usihojiwe?
Gesi ya Mnazi Bay, Mtwara iligunduliwa toka mwaka 1982 lakini mpaka
hivi sasa haijatumiwa kikamilifu. Kampuni ya Artumas ilianza utaratibu
wa kuichimba gesi mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18.
Tarehe 17 Oktoba 2007 kampuni ya Artumas ilitoa taarifa ya mpango wake
wa kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300. Mpango huu ulitarajiwa
kugharamiwa toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi – Netherlands
Development Finance Company.
Gharama za mradi wa kufua umeme
zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 225. Kampuni maalum ya kuendesha
mradi huu ya Tanzania Generation Company Ltd (TANGEN) ilisajiliwa ili
kujenga na kuendesha mradi huu.
Kampuni hii ingekopa dola milioni 160 na
dola milioni 65 zingechangiwa kama hisa na kampuni nyingine zikiwemo
mifuko ya pensheni ya Tanzania na kampuni ya madini ya Barrick
International.
Kampuni nyingine maalum ilitarajiwa kuanzishwa ili ijenge msongo wa
umeme (nguzo za nyaya za kusambaza umeme) na kuunganisha umeme wa Mnazi
Bay kwenye gridi ya taifa. Mradi huu ungegharimu dola milioni 400.
Mradi huu ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko ya pensheni ya Tanzania na
wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu ulikubaliwa na serikali
na ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme
(National Power Development Master Plan).
Mradi huu wa kufua umeme MW
300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco
inaueleza mpango huu kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali
iliukabali mradi huu baada ya kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.
Mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka 2008
uliathiri kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa moja ya Artumas
iliporomoka toka dola za Marekani 10.80 mwezi wa Aprili 2008 na kufikia
dola 0.12 mwezi wa Machi 2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa ya ukata
na ilibidi serikali iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na
ufuaji wa umeme wa MW 18 Mtwara. Barrick International ilijitoa katika
mradi wa TANGEN.
Katika kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc.
iliamua kubadilisha jina lake na kuwa Wentworth Resources Limited na
kuteua menejimenti mpya.
Tarehe 10 Juni 2009 Rais Kikwete alipokuwa anawahutubia Wabunge na
Wananchi katika Ukumbi wa Kilimani Dodoma kuhusu athari za mtikisiko wa
uchumi duniani alieleza “Kwa sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa
vitega uchumi kutoka nje umepungua.
Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha
kutoka mabenki na masoko ya mitaji.
Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa
kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa
ukuaji wa uchumi wetu na ajira.
Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule
Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake
haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium
smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani Mtwara, miradi ya
viwanda vya saruji na mbolea Mtwara.”
Kwa kauli ya Rais ambayo wananchi
wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla waliisikia kwani hotuba hii ilirushwa
live na Shirika la Utangazaji la Tanzania – Radio na Televisheni na
vyombo vingine vya habari.
Miradi ya kutumia gesi ni pamoja na kufua
umeme MW 300, kutengeneza mbolea inayotumia gesi kama malighafi,
aluminium smelter inayohitaji umeme mwingi, na kiwanda cha saruji
ambacho kinatumia umeme na kinu chake kinaweza kutumia gesi.
Wananchi
wakamuamini Rais wetu na wakaelewa kuwa miradi hii imekwama kwa sababu
ya mtikisiko wa uchumi na kwamba serikali inajitahidi kutafuta njia
mbadala ya kujikwamua ili miradi hiyo iendelee.
Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais Kikwete aliwaeleza
wananchi wa Mtwara akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara
itakayotumia gesi ya Mnazi Bay.
Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa
2010, ibara ya 63 kifungu (j) Kuzalisha umeme (300MW) kutokana na gesi
asili ya Mnazi Bay (k) Kupanua mitambo ya kusafisha gesi na bomba la
kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam. Mitambo ya kufua
umeme ya Dar es Salaam ilitegemewa itumie gesi ya Songosongo kwani
bomba la kutoka Songosongo hadi Somanga mpaka Dar es Salaam
lingepanuliwa.
Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq- Songas ilijiandaa
kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka Songosongo –
Somanga – Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya kufua
umeme Dar es Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi.
Serikali iliisitisha
kampuni hiyo isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa
umekamilika na kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau
MW 200.
Rais Kikwete alipoenda Mtwara kuhudhuria sherehe ya Mashujaa tarehe
25 Julai 2011 alizungumza na wananchi wa Mtwara na kueleza miradi ya
maendeleo itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay ikiwemo ufuaji
wa umeme wa MW 300 na kupanua bandari ya Mtwara.
Tarehe 12 Oktoba 2011, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari
kuwa “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni
mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme
ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa
haiko kwenye gridi hiyo.
Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka
makampuni ya China National Machinery&Equipment Import&Export
Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja
yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi
katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya
kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.
Mradi
huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za
Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye
nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC)
utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na
Serikali ya Tanzania.”
Mikoa sita ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa ni Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mradi huu pamoja na kufua umeme
wa MW 300 Mtwara ungekamilisha kuunganisha mikoa yote ya Tanzania
kwenye gridi ya taifa.
Taarifa iliendelea kueleza “Kuunganisha mikoa
yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa
zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na
kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo
itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.”
Maelezo haya yametolewa na Ikulu na vyombo vya habari vikayatangaza
na wananchi wa Mtwara wakasikia. Kutekeleza mradi wa kufua umeme
kutaifanya Mtwara iwe na umeme wa kutosha kushawishi kampuni kuanzisha
viwanda hasa ukizingatia ahadi ya Rais Kikwete ya kupanua bandari ya
Mtwara.
Mwaka wa fedha wa 2011/12 serikali ilitenga na kutumia shilingi
540 milioni fedha za maendeleo za mradi wa Mnazi Bay 300MW Development
Project.
Baada ya hapo mradi huu haukutengewa fedha tena. Badala ya
mradi huu kuendelezwa kama Rais alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na
Watanzania kwa ujumla badala yake wanasikia serikali imezindua mradi wa
kujenga bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Kwa taarifa ya Ikulu gharama za mradi wa kufua umeme wa MW 300
Mtwara na kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa gharama yake ni
dola milioni 684.
Mradi wa kutandaza bomba la gesi unagharimiwa na mkopo
wa dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export Import Bank ya China.
Ni
wazi gharama za kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa sita kwenye
gridi ya taifa ni ndogo zaidi kuliko gharama za kutandaza bomba la gesi.
Msongo wa umeme za kV 400 unajengwa kuunganisha Iringa – Dodoma –
Singida na Shinyanga.
Mradi huu unatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya
Afrika. Nyaraka ya mradi unaonyesha gharama za kujenga umeme za kV 400
ni dola za Marekani 600,000 kwa kilomita 1. Gharama za kujenga bomba la
gesi lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola 1,309,636 kwa kilomita 1.
Kwa madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga bomba la gesi ni zaidi
ya mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es Salaam.
Isitoshe unaweza kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusambaza kwa msongo
huo huo.
Ujenzi wa bomba la Dar es Salaam Mtwara umeanza bila kuwa na
mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha
hadi Dar es Salaam.
Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za
ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa
ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za
ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu.
Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33.7
imegunduliwa katika bahari yenye kina kirefu. Uchimbaji wa gesi hii bado
haujaanza.
Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya
uchimbaji wa gesi kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi bahari kuu bado
hazijafanya uamuzi wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha gesi hadi
nchi kavu.
Kwa kuwa gharama za kujenga bomba la gesi chini ya bahari ni
za juu sana, kampuni hizi zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu
kwenye eneo lililo fupi kuliko yote. Statoil imegundua gesi nyingi eneo
la Zafarani bahari kuu eneo la mkoa wa Lindi.
Hivi sasa wanatazama
maeneo ya Kilwa kuweza kuweka kituo cha nchi kavu. Bandari ya Lushungu
kata ya Limalyao, wilaya ya Kilwa ambayo ina kina kirefu cha bahari
yaelekea kuwavutia.
Kwa hivi sasa hakuna uhakika gesi iliyogunduliwa
bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa kujenga bomba kubwa umefanywa
haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida zake kiuchumi. Jambo la
kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na kuacha kutekeleza mradi wa
kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi, kijamii na uwajibikaji wa
kisiasa?
Wentworth Resources wamefanya upembuzi yakinifu (feasibility study)
na kubaini kwamba njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas
wanayoweza kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha
kutengeneza mbolea na kemikali nyingine Mtwara.
Kiwanda cha mbolea
chenye faida kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa hata kama akiba ya
gesi iliyogunduliwa siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay.
Mradi wa
kujenga kiwanda unaweza kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea
kiwanda kitazalisha methanol yenye soko kubwa duniani.
Kiwanda kitatumia
hewa ukaa (carbondioxide) na kwa hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha
mazingira. Uongozi wa Wentworth Resources una uzoefu wa miaka mingi
katika miradi ya kutumia gesi. Wanajua wanalolieleza. Hata hivyo
serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha kwenye bomba la gesi
la kwenda Dar es Salaam.
Serikali imeanzisha mgogoro wa gesi kwa kuanza kutekeleza mradi
mkubwa wa kutandaza bomba la mafuta na kuacha miradi yenye manufaa
makubwa kiuchumi na kijamii kwa taifa letu.
Uchunguzi huru na wa kina
ufanyike kubaini sababu za serikali kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara
na kukumbatia mradi wa kutandaza bomba. Ripoti aliyopewa Rais ya mradi
wa kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6 katika gridi ya taifa
itolewe ili Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi huu.
Mkataba wa
mkopo na utekelezaji wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe wazi.
Serikali iruhusu kampuni ya Wentworth resources kuendelea na mradi wa
kiwanda cha mbolea. Rais aende Mtwara kuwaeleza wananchi kuwa ahadi
alizoeleza za kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.
Vyama vya siasa na asasi za kiraia viruhusiwe kufanya mikutano ya
hadhara kueleza njia za kidemokrasia za kudai haki za kiuchumi za
wananchi wa Mtwara. Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza kwa nini
Mradi wa Kufua umeme MW 300 umesitishwa na serikali, upembuzi yakinifu
wa mradi wa bomba la gesi na mikataba yote inayohusiana na mradi huu.
Sakata hili la gesi ya Mtwara linaonyesha wazi kuwa hatuna sera
muafaka na mkakati wa kuendeleza sekta ya gesi kwa manufaa ya taifa letu
na Wananchi wa kawaida. Badala ya gesi kuwa neema inaelekea kuwa
itakuwa balaa na laana.
Sera ya gesi inapaswa kuweka taratibu
zitakazohakikisha kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hii na
utakaolinufaisha taifa letu bila kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye
teknolojia ya kutafuta na kuchimba gesi.
Wananchi wa Mtwara wanahitaji
kushirikishwa. Serikali iwe wazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi
ya gesi.
0 comments:
Post a Comment