MKUU wa Wilaya ya Arusha, John Mongela ametoa kauli ya serikali
kuwa Sekondari ya Korona haijafungwa kama ilivyotangazwa na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema kuwa mazingira yake hayawezi kutoa elimu
bora.
Mongela
alisema Lema hana nguvu ya kisheria kufunga shule, lakini akaahidi
kushirikiana naye kushughulikia changamoto zinazoikabili kama ambavyo
wamekuwa wakishirikiana.
“Naamini
mbunge ana nia njema, ila kwenye hili suala la kufunga shule amepotoka
kidogo, najua ni kiongozi aliyechanguliwa na wananchi wengi kutokana na
busara zake kutetea haki ila alipaswa atumie njia sahihi kurekebisha
makosa ya utendaji,” alisema Mongela.
Hata
hivyo, Mongela alimsimamsha kazi Mkuu wa shule hiyo, John Mbise
kutokana na kushindwa kutimiza wajibu, ikiwamo kwenda masomoni bila
kibali cha mwajiri wake.
Alisema
sheria namba 25 ya mwaka 1978, iliyofanyiwa mabadiliko katika sheria
namba 10 mwaka 1998, inatamka wazi wanaohusika kufunga shule ni
kamishna wa elimu, ofisa elimu mkoa, wilaya na viongozi wanaosimamia
ulinzi na usalama ngazi ya mkoa na wilaya.
“Nchi
yetu haiko kwenye vita na kuna mamlaka husika ambazo baada ya
kujiridhisha zinaweza kuchukua hatua za kufunga shule, lakini sivyo
alivyofanya mbunge ambaye ni mkazi wa Kata ya Engutoto na ameshiriki
kikamilifu wakati wa kuanzishwa kwake,” alisema.
Alisema
wabunge ndiyo watunga sheria. inashangaza kuona mbunge anakiuka misingi
ya sheria kwa kuchukua uamuzi kinyume na taratibu za uongozi.
Mongela
alimwagiza Ofisa Elimu Sekondari wa Jiji la Arusha, Violet Mlowosa
kuhakikisha Jumatatu wanafunzi wanafika shuleni bila kukosa na
atakayekosa bila sababu za msingi, atachukuliwa hatua za kisheria.
Pia, alitaka huduma ya maji kurejeshwa mara moja na deni wanalodaiwa kulipwa kwa Mamlaka ya Maji Arusha (Auwsa).
Alisisitiza
suala hilo kutofanywa kisiasa kutokana na umuhimu wake kwa jamii na
kumtaka ofisa elimu kupeleka majina ya watu waliopendekezwa kuunda bodi
ya shule hiyo.
Madhumuni
ya kujengwa shule hiyo yalikuwa iwe ya kidato cha tano na sita, lakini
hamashauri ya jiji ikabadili malengo hayo baada ya wanafunzi wengi
waliofaulu darasa kukosa nafasi.
Changamoto inayoikabili shule hiyo ni umbali wa takriban kilometa 16 kutoka katikati ya jiji.
0 comments:
Post a Comment