Angetile |
Na Boniface Wambura
KAMATI ya
Rufaa ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeahidi wadau wa
mchezo huo kuwa itafanya kazi zake kwa misingi ya haki.
Akizungumza
baada ya uzinduzi wa Kamati hiyo uliofanywa Dar es Salaam leo mchana (Januari
23 mwaka huu) na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba ya Rais wa TFF,
Leodegar Tenga, Mwenyekiti wa Kamati hiyo yenye wajumbe watano Idd Mtiginjola
amesema wapo kwa ajili ya kutenda haki.
Mtiginjola
amesema Kamati yao inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa
kuzingatia kanuni zilizopo na sheria nyingine za mpira wa miguu ikiwemo Katiba
husika.
“Niwakikishie
kuwa hatutafanya uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa kuzingatia
kanuni na sheria. Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo itafanya kazi zake kwa
kuzingatia sheria. Sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Sheria zipo kwa ajili
ya kuitafuta haki,” amesema Mtiginjola ambaye kitaaluma ni Mwanasheria akiwa ni
Wakili wa Kujitegemea.
Baada ya
uzinduzi, Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi (instruments)
mbalimbali zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, Katiba ya TFF
na Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mbali ya
Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis
Kabwe ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Rufani ya Tanzania, Kamanda wa Kikosi
cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP),
Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.
Mshambuliaji
wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni
Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini
Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa
Kaskazini.
Wakati huo
huo: Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kesho (Januari 24 mwaka huu) saa 6
kamili mchana litakuwa na mkutano na waandishi wa habari, ambao utafanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
0 comments:
Post a Comment