Msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ (kulia) akiwa na mama
yake, Luklesia Kalugila nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
baada ya kuachiwa huru kwa dhamana jana. Picha na Venance Nestory
HATIMAYE msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’
anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia amerejea uraiani jana
baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Lulu
anakabiliwa na shtaka la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven
Kanumba kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu. Aliachiwa kwa
dhamana jana saa 9:56 alasiri, baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa
ametimiza masharti.
Hadi
anaachiwa kwa dhamana jana saa 9:55 alasiri, msanii huyo alikuwa
ameshakaa mahabusu kwa miezi tisa, tangu alipokamatwa kwa tuhuma hizo,
Aprili 7, 2012.
Aliachiwa
baada ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Francis Kabwe kukagua na
kuridhishwa na nyaraka muhimu zilizohitajika kama sehemu ya masharti ya
dhamana na kutoa amri kwa msanii huyo kuachiwa huru kwa dhamana.
Dhamana
hiyo ilitolewa juzi lakini msanii huyo hakuweza kutoka gerezani
kutokana na Msajili wa Mahakama aliyepaswa kuthibitisha vielelezo vya
dhamana hiyo kutokuwepo mahakamani.
Akizungumza
huku akitokwa machozi muda mfupi baada ya kuachiwa, Lulu alimshukuru
Mungu, mawakili wake na watu wote waliokuwa wakimwombea katika mapito
yake hayo.
“Nawashukuru
watu wote. Watu waendelee kuniombea, hii ni dhamana tu lakini kesi bado
ni safari ndefu. Nawashukuru watu wote waliokuwa pamoja nami,
namshukuru Mungu kwani yeye ndiye kila kitu,” alisema Lulu.
Mmoja
wa mawakili wake, Peter Kibatala aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano
katika kufanikisha dhamana hiyo... “Sisi mawakili pamoja na Lulu
mwenyewe tunaishukuru sana Mahakama kwa kufanikisha haki hii ya msingi.
Msajili ametusubiri hadi sasa na hatimaye mchakato huu umetimia.”
Hali ilivyokuwa mahakamani
Lulu aliwasili mahakamani hapo saa 7:58 mchana akiwa kwenye gari la Jeshi la Magereza aina ya Landrover chini ya ulinzi.
Alipofikishwa,
alipelekwa katika mahabusu na baada ya takriban saa moja, aliingizwa
katika Ofisi ya Naibu Msajili, Kabwe huku akiambatana na wakili wake,
Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, wadhamini wake wawili na askari
Magereza.
Kabwe
alipitia masharti yote ya dhamana ikiwamo wadhamini wawili waliosaini
bondi ya Sh20 milioni kila mmoja. Bondi hiyo iliwekwa na Florian James
Mutafungwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Dk
Verusi Mboneko Kataruga wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Saa
9:26 alasiri alitoka katika ofisi hiyo na kurudishwa mahabusu ya
mahakama hiyo kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine za kimahakama
na za Jeshi la Magereza na baadaye aliingizwa masjala ya makosa ya
jinai kwa ajili ya kusaini hati ya dhamana.
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment