KUUAWA
kikatili kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi na
tukio la kutekwa, kuteswa kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini,
Dk. Steven Ulimboka, limechukua sura mpya ambapo sasa limetinga katika
Seneti ya Marekani, Tanzania Daima Jumamosi limeelezwa.
Taarifa kutoka Washington nchini Marekani zinasema Rais Jakaya
Kikwete amelalamikiwa rasmi katika Seneti na wanaharakati na watetezi
wa haki za binadamu nchini, na kwamba masuala hayo sasa yatafikishwa
kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binadamu (UNHRC)
kwa hatua zaidi.
Mbali na mauaji ya Mwangosi na tukio la Dk. Ulimboka, Rais Kikwete
pia amelalamikiwa kwa kufumbia macho matukio mengi ya kuteswa na kuuawa
kwa raia pamoja na kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la uchunguzi la
MwanaHalisi, kutoroshwa wanyama hai kwa kupelekwa nje ya nchi na hatua
ya polisi kutumia silaha za kivita kupambana na raia wasio na silaha
wakiwemo wanafunzi wanaoandamana.
Ripoti hiyo ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu yenye
kurasa 27, inatuhumu utawala wa Rais Kikwete kwa kukandamiza demokrasia
kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya dola.
Watetezi hao wa haki za binadamu, wamedai kuwa baada ya kufanikiwa
kuingiza masuala haya ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika Seneti ya
Marekani, sasa wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha suala hili
linafikishwa Umoja wa Mataifa kwa kile walichokiita, kuiadabisha
serikali.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana, na pia kusambazwa katika
baadhi ya taasisi za habari, suala hilo liko mikononi mwa Seneta Kerry,
ambaye baada ya majadiliano katika Seneti, ripoti hiyo itapelekwa UNHRC.
Habari zinasema baadhi ya wajumbe wa Seneti waliofanikiwa kuona
ripoti hiyo wamemeshitushwa na kile walichokishuhudia katika picha
zilizoambatanishwa.
Aidha, ripoti hiyo pia imeeleza jinsi rushwa ilivyoshamiri nchini,
ukandamizaji juu ya uhuru wa maoni na matumizi mabaya ya vyombo vya
dola kudhibiti vyama vya upinzani na kutumia silaha za kivita kupambana
na raia wasio na silaha.
Ripoti hiyo ya kuishitaki Serikali ya Kikwete, pia imelaani vitendo
vya polisi kusambaratisha maandamano ya wanafunzi wa shule za msingi
jijini Dar es Salaam, walioandamana Julai 31, mwaka jana kupinga
ukosefu wa walimu nchini.
Mgomo wa wanafunzi ulikuja baada ya walimu wa shule za msingi na
sekondari kupitia jumuiya yao - Chama cha Walimu Tanzania (CWT) –
kuitisha mgomo nchi nzima wa kutaka kuboreshwa kwa mazingira ya kazi
zao, nyongeza ya mishahara na malimbikizo ya posho.
Nyaraka zilizowasilishwa na wanaharakati hao, zimeambatanishwa na
picha zinazoonesha namna Jeshi la Polisi lilivyohusika kuuawa kwa
Mwangosi, picha mbaya ya maiti ya mwanahabari huyo, na namna Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alivyokuwa akishuhudia
askari wake wakimsulubu mwanahabari huyo kabla ya kufunga kazi kwa
kumaliza uhai wake.
Kadhalika, kumeambatanishwa picha zinazoonesha maiti za watu
waliouawa wakati wa maandamano huko Arusha, na ile inayosadikiwa
kutokea kule Songea. Picha nyingine za kusikitisha ni zile zinazoonesha
askari zaidi ya watano wakimdhibiti mwanaharakati mmoja katika
maandamano, na umati wa wanafunzi wa shule za msingi wakiandamana, huku
nyingine zikionesha askari mwenye silaha ya kivita akimsindikiza
mwanafunzi wa kike mwenye mfuko wa madaftari.
Tangu mwaka 2005 ambapo masuala mazito ya rushwa yamekuwa
yakiibuliwa, ikiwamo ununuzi wa rada feki, wizi wa fedha za umma kutoka
kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), mkataba tata wa Richmond, ukusanyaji wa kodi, utoroshwaji wa
wanyama hai, wizi wa nyara za serikali, ikiwamo pembe za ndovu, baadhi
ya wananchi wamekuwa wakituhumu serikali kushindwa kuchukua hatua.
Vilevile, wananchi wamekuwa wakituhumu Serikali ya Kikwete,
kukumbatia wezi wa fedha za umma katika halmashauri za miji na wilaya,
uporaji wa ardhi unaofanywa na makampuni makubwa ya ndani na nje ya
nchi.
Jana, Tanzania Daima Jumamosi haikufanikiwa kumpata Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu kuzungumzia iwapo serikali ina
taarifa juu ya jambo hili kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita muda wote
bila kupokelewa.
Kova ajivua
Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova jana
ametangaza rasmi kujivua katika sakata zima la kuchunguza kutekwa na
kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka.
Aidha, Kova pia amekanusha madai ya kuunda tume kuchunguza suala
hilo, akitaka asiulizwe jambo lolote, huku akisukuma tukio hilo kwa
wakubwa wake.
Juzi, Kamanda Kova aliliambia Tanzania Daima kwamba, jana angeweka
wazi suala hilo ili Watanzania wajue kilichojiri kuhusiana na kutekwa
na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, jambo ambalo limetikisa anga, likiwemo
lile la kukamatwa kwa raia wa Kenya, Mulundi anayedaiwa kuhusika na
tukio hilo.
Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, jana Kamanda Kova
aliruka kimanga na kudai kwamba wenye uwezo wa kulitolea maelezo ni
wakuu wake wa kazi, kwa maana ya Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini.
Kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza utekaji huo, Kova alisema
kilichofanyika wakati huo ni kuundwa kwa jopo la uchunguzi ambalo
taarifa zake hazina ulazima wa kutolewa mbele ya jamii zaidi ya
kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa kile walichokibaini.
Alisema baada ya kukamilisha kazi yake, alipeleka jukumu la
kupeleleza sakata hilo katika ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai
nchini (DCI) ambayo ndiyo yenye jukumu la kutoa maelezo.
chanzo: Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment