WATU 21 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tanganyika, baada ya
boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama baada ya kupigwa na
mawimbi.
Taarifa
za tukio hilo lililotokea juzi usiku zinaeleza kwamba boti hiyo
inayojulikana kwa jina la Yarabi Tunusuru, ilikuwa imebeba abiria 85,
ambapo 64 kati yao waliokolewa.
Katika
harakati za uokoaji, miili ya watu tisa waliokufa maji iliopolewa na
watu 12 hawajulikani walipo huku hofu ikitanda kuwa wamefariki dunia.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai alithibitisha kutokea kwa
ajali hiyo akisema ilitokana na uzembe wa kiongozi wa boti, kutosikia
malalamiko ya abiria.
Nahodha
wa boti hiyo, Akilimali Seif, alisema kuwa walianzia safari yao katika
Kijiji cha Kipili mkoani Rukwa, Jumatano iliyopita, kuelekea Mji wa
Uvira uliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alisema
kuwa ikiwa njiani, boti hiyo ilikuwa ipitie mji wa Rumonge nchini
Burundi, ambako ingeshusha sehemu ya mzigo iliyobeba ambayo idadi kubwa
ilikuwa ni chakula.
“Tulianza
safari salama tukienda Uvira, DRC kupitia Burundi katika mji wa
Rumonge, kupeleka mizigo ya wafanyabiashara. Lakini, hali ilianza
kubadilika juzi (Alhamisi),” alisema nahodha huyo na kuongeza:
“Saa
nane mchana tukiwa Kijiji cha Kalilani (kilichopo jirani kabisa na
Hifadhi ya Taifa ya Mahale), mvua kubwa ilinyesha na mawimbi yakawa
makubwa. Kwa kweli siamini kama baadhi yetu tumeokoka.”
Alifafanua:
“Kilichosababisha boti yetu ipasuke ni ubishi wa aliyekodi; … Licha ya
abiria kumlalamikia wakitaka aegeshe boti ufukweni, yeye alikataa na
kulazimisha tuendelee na safari. Matokeo yake mawimbi yakazidi, hadi
ilipofika saa nne na nusu usiku injini ya boti ilizimika, ndipo maji
yakawa yakiingia.”
Seif aliendelea kuhadithia kuwa maji yaliendelea kutanda kwenye boti na muda mfupi baadaye ilipasuka na kuzama.
Alisema
kwamba kabla ya kupasuka, boti hiyo ilikuwa ikisukumwa na mawimbi
kuelekea eneo la ufukweni mwa ziwa, ambapo abiria walianza kuweweseka
na kila mmoja akawa anatafuta cha kumwokoa.
Kwa
mujibu wa Seif, wachache walibahatika kuvaa majaketi ya uokoaji
yaliyokuwapo na wengine ilibidi wajaribu kutumia mapipa ya mafuta,
matenga ya samaki na magunia ya mihogo.
0 comments:
Post a Comment