RAIA
wa Kenya, Joshua Mulundi, anayekabiliwa na kesi ya kumteka na kutaka
kumsababishia kifo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini,
Dk. Steven Ulimboka, ameanza mgomo wa kula na ameamua kuishi juu ya paa
la Gereza la Keko akitishia kutaka kujiua.
Mtuhumiwa huyo ambaye Jumapili iliyopita kupitia gazeti la Tanzania
Daima Jumapili alitoboa siri ya jinsi alivyokamatwa na kutoa kauli
nzito kulalamikia mwenendo wa kesi yake, amefikia hatua hiyo kwa lengo
la kuishinikiza serikali imlete mbele yake Dk. Ulimboka ili afanyiwe
gwaride la utambulisho kubaini kama alihusika katika tukio la kumteka.
Akizungumza na gazeti hili juzi kutoka ndani ya Gereza la Keko,
Joshua alisema kuanzia jana alitarajia kuanza mgomo wa kutokula na
atakuwa akiishi juu ya paa la gereza hilo kwa lengo la kuishinikiza
serikali ikamilishe uchunguzi wa kesi yake.
Habari kutoka ndani ya Gereza la Keko ambako mtuhumiwa huyo amehifadhiwa, zilisema kuwa raia huyo wa Kenya ameanza mgomo jana.
Imeelezwa kuwa amechukua uamuzi huo mgumu baada ya kutoridhishwa na
mwenendo wa kesi ambayo tangu Julai 3, mwaka jana bado iko kwenye hatua
ya upelelezi na hajui utakamilika lini.
Askari mmoja wa Jeshi la Magereza kutoka ndani ya gereza hilo
alikiri kuwa mtuhumiwa huyo amegoma na usiku wa kuamkia jana alishinda
juu ya paa la gereza huku mvua ikimnyeshea.
“Ni kweli huyo bwana amegoma, uongozi wa gereza umefanya juhudi za
kuzungumza naye na kilio chake anasema anataka upelelezi wa kesi yake
ukamilike haraka ili atendewe haki, lakini kubwa kuliko yote, ameitaka
serikali imlete Dk. Ulimboka mahakamani ili aweze kumtambua,” alisema
askari huyo.
Habari zaidi zinasema kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambaye hana
wakili mahakamani, wamewasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kutoa
msaada wa kisheria.
Kwa mujibu wa ndugu hao, hadi sasa hawaoni maendeleo ya kesi hiyo
kwani kila ikifika mahakamani upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka
iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.
Juzi mtuhumiwa wa kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini
aliliambia gazeti hili kuwa amepata kutoa malalamiko kwa Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali
imlete mbele yake, Dk. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi
wa kesi hiyo unafikia tamati.
Mbali ya maombi hayo, mtuhumiwa huyo pia alisema aliwaomba viongozi
hao wamsaidie kupata dhamana kwani kesi inayomkabili inaruhusu dhamana
na hana wakili wa kumtetea.
Dk. Ulimboka ajipa muda
Wakati Joshua akitaka afanyiwe gwaride la utambulisho, kwa upande
wake Dk. Ulimboka alisema kwa sasa hana cha kusema, lakini muda ukifika
atasema ukweli wote.
Alisema hajawahi kuitwa na kukutanishwa na mtuhumiwa wa kesi hiyo
wala hajaombwa kuwa mmoja wa mashahidi, ingawa anajua atatakiwa kwenye
ushahidi.
“Mimi sina la kusema kwa sasa, naviachia vyombo husika kufanya kazi
yao, lakini muda ukifika naweza kusema lolote, ila kwa sasa tuviachie
vyombo vya dola,” alisema Dk. Ulimboka.
Magereza wang’aka
Kwa upande wake, Jeshi la Magereza nchini limegoma kuzungumzia mgomo
wa mahabusu huyo na hatua anazochukua gerezani kushinikiza kesi yake
iendeshwe haraka.
Msemaji wa jeshi hilo, Danstan Lissu, alipoulizwa na gazeti hili
alikuwa mbogo na kuhoji gazeti hili limepataje taarifa za mgomo wa
mahabusu huyo.
“Taarifa hizi umepata wapi? Nani amekuambia? Siwezi kulizungumzia
suala hilo kwa vile sijaruhusiwa, mtafute Kamishna Mkuu wa Magereza
akupe taarifa hiyo,” alisema Lissu.
Hata hivyo Tanzania Daima Jumatano ilipomtafuta Kamishna Mkuu wa
Magereza, John Minja, kupata taarifa juu ya mahabusu huyo hakuweza
kupatikana na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu.
Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa
nchini kwa wakati tofauti mwaka jana; alitekwa, kuteswa, kupigwa hadi
kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova, alitangaza kuunda tume ya wataalamu kutoka ndani
ya jeshi hilo, iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja baadhi
ya watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini hadi
sasa Mulundi ndiye mtuhumiwa pekee aliyekamatwa.
Hata hivyo tume hiyo haijawahi kutoa ripoti yake kama Kova
alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka
hajawahi kuhojiwa, huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira
kuhusiana na sakata hilo.
Hivi karibuni jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso,
limekanusha kuwapo kwa tume hiyo, likisema walioteuliwa ni polisi ambao
watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za polisi.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye hivi karibuni
alikiri kuwapo kwa tume hiyo, lakini akasema hawezi kulizungumzia suala
hilo kwa vile taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu
baada ya kukamilisha wajibu wake.
Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk.
Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo
yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi.
Katika tamko lake mwishoni mwa mwaka jana lililosomwa kwa niaba
yake na wakili wa kujitegemea, Nanyoro Kicheere, akimwakilisha
mwanasheria wake, Dk. Ulimboka alisema wapo watu ambao hawatapenda
kusikia siri iliyojificha katika tukio zima la kutekwa kwake na kwamba
hana jinsi zaidi ya kueleza ukweli wakati ukifika.
Alisema kuwa tukio la kutekwa na hatimaye kutupwa katika msitu wa
Mabwepande, lilitokea wakati akiwa katika kikao na ofisa
aliyetambulishwa kwake kuwa ni Ofisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid Ighondu,
ambaye hadi leo Ikulu haijatoa ufafanuzi kama inamtambua au la.
chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment