Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) imeahirisha uchaguzi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania
(TAFCA) uliokuwa ufanyike leo (Januari 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Uchaguzi umeahirishwa kwa vile ulitaka kufanyika bila
kuzingatia Katiba ya TAFCA Ibara ya 32(1) na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa
TFF Ibara ya 10(6) na 26(2), hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeahirisha
uchaguzi huo kwa vile nafasi zilizoombwa kugombewa na idadi ya waombaji uongozi
haikidhi matakwa ya Katiba ya TAFCA.
Pia taratibu za kikanuni ikiwa ni pamoja na kuwaarifu
waombaji uongozi ambao hawakukidhi matakwa ya Katiba ya TAFCA hazikukamilika
kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Licha ya upungufu huo, TAFCA haikuwasilisha taarifa za
mchakato mzima kama ilivyoombwa na TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza
Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA kuandaa uchaguzi mpya utakaokidhi matakwa ya Kamati
ya TAFCA baada ya Uchaguzi Mkuu wa TFF.
TFF inaishauri TAFCA kutumia fursa ya Mkutano Mkuu wa leo
(Januari 19 mwaka huu) kujadili mustakabali wa TAFCA kwa kuwa chama hicho
kimeshindwa mara mbili kupata idadi ya wagombea wanaokidhi akidi ya Kamati ya
Utendaji.
Pia TAFCA haijawahi kufanya mikutano ya Kamati ya Utendaji
na Mkutano Mkuu kwa karibu miaka minne.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment