Rage kulia akiwa na rais wa Etoile, kushoto na Okwi katikati jana baada ya kumaliza biashara mjini Tunis, Tunisia |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Simba imesema kwamba haitafanya haraka kuziba nafasi
ya mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uganda, Emannuel Okwi iliyemuuza Etoile du
Sahel ya Tunisia jana.
Hans Poppe |
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans
Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba kwa kuwa wamekwishakamilisha usajili
wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika na muda wa kusajili unaisha leo, hawatafanya
haraka ya kusajili mchezaji mwingine.
“Daima sisi huwa tunasajili kwa makini na matunda yake ni
kuuza wachezaji kwa bei nzuri, mfano Patrick Ochan, Mganda mwingine tuliyemuuza
TP Mazembe (ya DRC), hivyo hatutafanya papara tena katika kusajili, ili tupate
mkali kama au zaidi ya Okwi,”alisema Poppe.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
alisema kwamba watasubiri kuona kama watafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya
Mabingwa Afrika ndipo wasajili mchezaji mwingine, vinginevyo itakuwa hadi msimu
ujao.
Simba jana ilimuuza Okwi klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia
kwa dau la dola za Kimarekani 300,000, zaidi ya Sh Milioni 450 za Tanzania.
Okwi, aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 aliisajiliwa Simba
akitoea SC Villa ya Uganda mwaka 2010 akiwa kinda wa miaka 17, akisajiliwa kwa
dau la dola za Kimarekani 40,000.
Baada ya kumaliza mkataba wake wa awali, Desemba mwaka jana
aliongeza mkataba wa miaka miwili na Simba SC ambao kabla hajaanza kuutumikia,
anahamia Sahel.
ALIYEMTOA JASHO TENGA 2008 ACHUKUA FOMU LEO URAIS TFF
Malinzi kushoto akiwa na Tenga katika uchaguzi uliopita TFF |
Na Mahmoud Zubeiry
JAMAL Emil Malinzi, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA),
anatarajiwa kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) leo mchana, makao makuu ya shirikisho hilo, Ilala mjini Dar es
Salaam.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwa
watu wa karibu wa Katibu huyo wa zamani wa klabu ya Yanga, zimesema kwamba
Malinzi atachukua fomu mchana wa leo.
Katika uchaguzi uliopita wa TFF uliofanyika Desemba 14, mwaka
2008, Malinzi alikuwa mpinzani mkuu wa rais anayemaliza muda wake, Leodegar
Chillah Tenga ambaye amekwishatangaza hagombei tena.
Katika uchaguzi huo, uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water
Front, Dar es Salaam, Tenga alishinda kwa kura 64 kwa 39.
Awali, Malinzi alienguliwa kwa kigezo cha uzoefu, lakini
akarejeshwa kuwania nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake.
Katika uchaguzi huo ulioshuhudiwa na Mwakilishi wa FIFA,
Ashford Mamelodi, Athumani Nyamlani alishinda nafasi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais, baada ya kujikusanyia kura 65 kati ya kura 107 zilizopigwa na kura mbili
kuharibika, akimshinda Lawrence Mwalusako aliyepata kura 39 na Ali Mwanakatwe
aliyeambulia kura moja.
Nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, ambayo kwa sasa imefutwa, ilikwenda
kwa Ramadhani Nassib aliyemwangusha mpinzani wake wa karibu, Damas Ndumbaro
aliyepata kura 45.
Hadi sasa, mbali na Malinzi mgombea mwingine anayetarajiwa
katika nafasi ya Urais ni Athumani Nyamlani, Makamu wa kwanza wa sasa wa Rais
wa TFF.
Jumla ya watu 26 hadi jana walikuwa wamekwishachukua fomu za
kugombea nafasi mbalimbali, kuelekea uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Februari
24, mwaka huu.
Hata hivyo, idadi hiyo ni kwa wale wanaochukua fomu hizo
katika ofisi za TFF, kwani vilevile zinapatikana kupitia tovuti ya TFF ya
www.tff.or.tz ambapo mwisho wa kuchukua na kurejesha ni saa 10 kamili alasiri
Januari 18 mwaka huu.
Waliochukua jana ni Michael Wambura anayewania umakamu wa
rais wakati kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Mbasha Matutu, Muhsin
Balhabou, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder.
Idadi kamili ya waliochukua ni Michael Wambura, Ramadhan
Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais). Kwa upande wa wajumbe na kanda zao
kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel
Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles
Mugondo, Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo
(Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya
(Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma).
Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart
Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed
(Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder
(Dar es Salaam).
Naye Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania umakamu
mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
0 comments:
Post a Comment