.

.
Thursday, December 13, 2012

10:20 PM
Mwaikimba kulia na Hajji Nuhu kushoto; wamo safarini na Azam DRC

Na Mahmoud Zubeiry
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, (CAF), Azam FC wanaondoka mchana wa leo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kucheza mashindano ya Kombe la Hisani.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza leo na itafikia tamati Desemba 23, mwaka huu na Azam FC itashiriki kwa lengo la kuwapa mazoezi na uzoefu wachezaji wake kabla ya kuingia kwenye Kombe la Shirikisho mwakani.
Azam pia, itatumia mashindano hayo kama fursa ya kuwapima wachezaji wake kabla ya kuanza kwa Kombe la Shirikisho mwakani, ambako wamepangwa kuanza na Al Nasr Juba ya Sudan Kusini.
Hata hivyo, katika kikosi cha Azam kitakachoondoka leo, hawamo wachezaji wake wapya wa kigeni, iliyowasajili beki Mkenya, Joackins Atudo na mshambuliaji Mganda, Brian Umony.
Mashindano hayo yatashirikisha timu kubwa za kutoka Kongo kama DC Motema Pembe na A.S. Vita Club, wakati timu kutoka nje ya Kongo mbali na Azam FC, kuna Tusker FC ya Kenya, Gombe United ya Nigeria na Diable Noirs ya Kongo Brazzaville.
Kikosi cha Azam kinachokwenda DRC ni; Mwadini Ally, Jackson Wandwi, Gaudence Mwaikimba, Himidi Mao, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Kipre Tchetche, Kipre Balou, Luckson Kakolaki, Samir Hajji Nuhu, Zahoro Pazi, Seif Abdallah, Malika Ndeule, Omar Mtaki, Abdi Kassim, Uhuru Suleiman na David Mwantika.
Wachezaji wengine ambao hawahusiki katika safari hiyo, ni wale waliopo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco ‘Adebayor’ na Salum Abubakar, wakati wengine ni waliosimamishwa kwa tuhuma za kuhujumu timu, Aggrey Morris, Deo  Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni ambao wote wapo timu ya taifa pia na Said Mourad.
Kikosi hicho kitaongozwa na kocha Mkuu, Muingereza Stewart Hall.

0 comments:

Post a Comment