.

.
Friday, December 21, 2012

11:08 AM
Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Harison Mwakyoma  akiongea na madereva wa Boda Boda kwenye mkutano uliofanyika katika uwanja wa wazi uliopo kata ya kimandolu jijini Arusha.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Katika kile kinachoonekana kuhamasisha madereva wa pikipiki za abiria maarufu kama boda boda kupata mafunzo yao kupitia vyuo, jeshi la Polisi mkoa wa Arusha kupitia kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na baadhi ya vyuo vya udereva wameanza kutoa mafunzo kupitia ofisi za kata.
Neema hiyo ilitangazwa juzi kwa Madereva hao na Mkuu wa Kikosi hicho Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Harison Mwakyoma alipokuwa anazungumza nao katika mkutano uliofanyika kiwanja cha kata Kimandolu.
Alisema kwamba ameamua kuongea na baadhi ya wamiliki wa vyuo vya udereva vilivyopo mkoani hapa ili watoe mafunzo hayo kwa madereva kwenye kata zao tena kwa gharama ya chini Kabisa ambayo ni Tsh 30,000 tu hali ambayo itasaidia kutoa hamasa kubwa kwa madereva hao kujifunza.
“Pamoja na kujua kuendesha pikipiki ila hamjui sheria za usalama barabarani, mafunzo yatawasaidia sana, mbali na kujua sheria za usalama barabarani ambazo zitawasaidia kuepusha ajali pia yatawasaidia kujua haki zenu”.  Alisema Mwakyoma.
Aliongeza kwa kuwaambia kuwa siku zote wakitaka wasifuatiliwe na askari wanatakiwa wawe wametimiza vigezo vyote wanapokuwa barabarani kama vile kuwa na leseni ya udereva, kofia ngumu “Helmet” n.k.
Mkuu huyo wa Usalama barabarani amesema ameanzisha kampeni hiyo ili kila mmoja apate mafunzo yake kupitia chuo hali ambayo itasaidia kupunguza ajali za barabarani kwa kiasi kikubwa.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi Gilles Muroto, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi toka Dawati la Jinsia na Watoto, Maria Maswa, Polisi tarafa, viongozi wa tarafa ya Suye, kata, mitaa na madereva wapatao 100.
Mkutano huo pia ulitawaliwa na makofi ya pongezi pamoja na vifijo kutoka kwa madeva hao baada ya Mkuu huyo wa Usalama Barabarani kuwaahidi kuwa kama wangekuwa tayari hata siku ya pili yake (jana) wangeweza kuanza darasa.
Alimalizia kwa kuwaasa madereva hao kutojichukulia sheria mkononi pindi mwenzao anapogongwa na gari kwani vitendo hivyo vinaweza kuwagharimu badala yake aliwataka wafanye mambo manne muhimu; kwanza kuandika namba ya gari iliyosababisha ajali, kuielewa mahali ajali ilipotokea, kutoa taarifa polisi na mwisho kumwahisha mwenzao hospitali.
Programu ya mafunzo kwa waendesha pikipiki mkoani hapa ilianza rasmi mwezi Agosti mwaka huu baada ya kufunguliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la ajali.
Hali hiyo imesaidia sana kupunguza kiwango cha ajali mkoani hapa toka wastani wa ajali 5 za boda boda kwa wiki hadi moja au kutokuwepo kabisa.
Hadi sasa waendesha boda boda wapatao 900 kutoka wilaya za Arusha mjini, Arumeru na Monduli wamekwisha pata mafunzo ya udereva toka vyuo mbalimbali vilivyopo mkoani hapa.

0 comments:

Post a Comment