.

.
Sunday, December 2, 2012

2:17 PM

            Rais wa Kenya, Mwai Kibaki amewaaga rasmi wakazi wa Arusha na Watanzania wote kwa ujumla wakati akihitimisha kazi yake ya mwisho mjini hapa akiwa kama mwenyekiti wa marais wa jumuiya ya Afrika Mashariki.


Kazi ya Mwisho ya Rais Kibaki ilikuwa ni kulizindua jengo jipya la makao makuu ya Jumuiya hiyo iliyofanyika hivi karibuni mjini Arusha, lililojengwa kwa thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 26, zikiwa ni sehemu ya bilioni 30 zilizotolewa kama ufadhili wa serikali ya Ujerumani kwenye jumuiya hiyo.


 Rais Kibaki anatarajiwa kumkabidhi Rais Yoweri Museveni uenyekiti wa Marais wa nchi tano za jumuiya katika mkutano wa mwaka wa viongozi hao utakaoanza hivi karibuni jijini Nairobi nchini Kenya.


 Kiongozi huyo wa Kenya ambaye amesisitiza umoja wa wananchi wa nchi zote tano za jumuiya ya Afrika Mashariki, anatarajiwa pia kuachia rasmi, Urais wa Kenya mwezi wa tatu mwakani baada ya uchaguzi utakaomsimika kiongozi mpya wa taifa hilo.


"Jumuiya yetu imepanuka kutoka kwenye uanachama wa nchi tatu hadi tano za sasa, na jengo hili ndiyo kielelezo cha umoja wetu," alisema Kibaki katika uzinduzi huo wa majengo mapya ya makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki.





Mapema akilihutubia bunge la Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete alitahadharisha kuwa Jumuiya hiyo isikimbilie kwenye umoja wa sarafu kabla kwanza kufanya utafiti wa kutosha juu ya jambo hilo





Aidha wakuu wa nchi za jumuia ya afrika mashariki, (EAC).hivi karibuni walizindua rasmi  majengo mapya ya makao makuu ya jumuia hiyo yaliyopo mjini Arusha ambapo Katika hafla hiyo fupi, Marais 5 walishiriki katika uzinduzi huo.


 Marais hao walioshiriki ni pamoja na Mwai Kibaki wa Kenya, Jakaya Kikwete wa Tanzania, piere Nkurunzinza wa Burundi, Paulo Kagame wa Rwanda na Yoweri Mseveni wa Uganda.





Uzinduzi huo unaiwezesha jumuia hiyo kuwa na majengo yake tangia izinduliwe kwa mara ya pili mwaka 1998 ,ambapo awali ilikuwa imepanga katika majengo ya kituo cha mikutano ya kimataifa AICC.


 Mara baada ya uzinduzi wa majengo hayo, viongozi hao pia walizindua bara bara ya Athe river inayounganisha nchi za Tanzania na Kenya kutokea  Nairobi hadi Namanga nchini Tanzania .


 Aidha Bara bara hiyo ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na jumuia ya Afrika mashariki kwa ufadhili wa  benki ya maendeleo ya Afrika, ADB kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano ya bara bara katika nchi za jumuia ya afrika mashaiki

0 comments:

Post a Comment