.

.
Thursday, December 13, 2012

10:23 PM
Brandts

Na Mahmoud Zubeiry
ERNIE Brandts anabakia kuwa kocha ‘baab kubwa’ zaidi kati ya makocha wanaofanya kazi Tanzania, licha ya Simba SC jana kumtaja kocha wake mpya, Patrick Liewig kutoka Ufaransa anayerithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick aliyetimuliwa.
Kwa mujibu wa wasifu wa mtaalamu huyo, aliyezaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na kuichezea PSV Eindhoven ya Ligi Kuu ya Uholanzi, pia alichezea Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, kabla ya kutua Yanga mwaka huu.
Kwa upande wake Liewig, ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, Patrick Liewig ndiye atakayerithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick katika klabu ya Simba.
Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Patrick Liewig
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kim Poulsen
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
Kocha mwingine Mzungu Tanzania ni Muingereza John Stewart Hall anayeifundisha Azam FC kwa sasa.
Hall alikuwa Mkurugenzi wa akademi ya Birmingham City F.C. na amewahi kuzifundisha Saint Vincent na Grenadines na Pune FC ya India.
Brandts ni baab kubwa hata mbele ya kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen. Sifa kuu ya Poulsen ni kuiongoza Viborg FF kutwaa ubingwa wa Kombe la Denmark mwaka 2000.
Poulsen alicheza soka ya ridhaa tu na alipata heshima ya kitaifa kama kocha, alipoiongoza Aarhus Fremad kutwaa mataji matano ndani ya miaka tisa, kuanzia 1987 hadi 1995.
Aliifundisha pia AC Horsens kuanzia 1996 hadi 1997 kabla ya kurejea Aarhus Fremad mwaka 1998. Aliifundisha tena AC Horsens mwaka 1999, kabla ya kutimkia Viborg FF mwaka huo huo.
Chini ya Poulsen, Viborg FF ilikuwa moto na ikatwaa taji la Kombe la Denmark mwaka 2000 pamoja na Super Cup ya nchini humo. Oktober 2001, Poulsen alifukuzwa kisha baadaye akaenda kufundisha Randers FC.
Desemba mwaka 2002, Poulsen alitimkia Singapore, ambako alifundisha Under-18, kabla ya kurejea Denmark, alipojiunga na Vejle Boldklub Januari 2006 kwa mkataba wa mikaka mitatu. Alifukuzwa katika klabu hiyo Aprili mwaka 2007, na akaenda kujiunga na Naestved BK Julai mwaka huo huo.
Juni 2010 aliteuliwa kuwa kocha wa FC Hjorring, ambako aliacha mwenyewe kazi, baada ya kupata mkataba wa kufundisha timu za vijana za Tanzania, Aprili mwaka jana na Mei mwaka huu akapandishwa kuwa kocha wa timu ya wakubwa, Taifa Stars akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Borge Poulsen.
Kulingana na wasifu wa makocha hao, Brandts anendelea kuwa kocha aliyetamba zaidi, kuanzia kucheza Kombe la Dunia na kufundisha timu kubwa Ulaya. 
Stewart Hall

0 comments:

Post a Comment