.

.
Saturday, December 15, 2012

1:03 AM
CHAMA cha Demokarasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Chato mkoani Geita, kimemshukia Mkuu wa Polisi wilayani humo, Leonard Nyaoga kwa madai kuwa anatumiwa na CCM kutaka kudhoofisha jitihada zao.
Tuhuma hizo zimekuja kufuatia OCD huyo kuualifu uongozi wa CHADEMA kwa njia ya simu kuwa amesitisha mikutano yao ya hadhara kwa madai tayari walikwisha kukaa kikao cha pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na dini na kukubaliana kuisitisha.
Hata hivyo sababu hizo zilipingwa vikali na CHADEMA kwa madai kuwa katika kikao cha pamoja na jeshi hilo Nevemba 7 mwaka huu, ilizuiliwa mihadhara ya kidini na wala si mikutano ya vyama vya siasa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa CHADEMA wilaya ya Chato, Mange Ludomya, alisema kitendo cha OCD kuzuia kuendelea na mikutano yao kinaonyesha wazi jinsi anavyoweza kuwa anatumiwa na chama tawala kuwadhoofisha.
"Tunamshangaa sana huyu OCD wetu...sisi tulipeleka barua ya kumtaarifu kuwa tutakuwa na mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Nyarututu kata ya Bwanga Desemab 16 kama sheria inavyotuagiza lakini amenipigia simu ananieleza kuwa mkutano huo usitishwe kwa kuwa tulikubaliana,” alisema.
Kufuatia hali hiyo, Katibu huyo alisisitiza kuwa mikutano ya CHADEMA itafanyika kama kawaida na kama ni nguvu za jeshi la polisi ni bora zikatumika kusaka majambazi wenye silaha zinazoangamiza maisha ya wananchi.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo alikana kuwepo kwa zuio hilo na kudai kuwa zuio kama hilo hufanyika kwa maandishi si kwa njia ya simu.
Aidha, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kunapotokea mkanganyiko kama huo ni vema wakawasiliana na wenzao ngazi ya mkoa kwa lengo la kumfikia ofisini kwake na kufanya mazungumzo ili kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza.
chanzo: tanzania daima

0 comments:

Post a Comment