.

.
Tuesday, December 18, 2012

10:23 PM
Kikosi cha Azam

Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
AZAM FC inashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Martyrs, kumenyana na Real De Kinshasa ya hapa, katika mchezo maalum wa kutafuta timu ya kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Hisani mjini hapa, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka DRC.
Real imeshika mkia katika Kundi A, wakati Azam pia imeshika mkia katika Kundi B, hivyo zinamenyana leo kuwania tiketi ya Nusu Fainali.  
Azam juzi ilifungwa mabao 2-0 na Shark FC ya hapa, katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi B, Kombe la Hisani, kwenye Uwanja wa Martyrs jioni hii.
Mabao ya washindi, timu inayomilikiwa na mdogo wake rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila yalifungwa na Ndibu Kalala dakika ya 23 na Kalala Kabongo dakika ya 34.
Hata hivyo, kipigo hicho kilichangiwa kwa kiasi kikubwa na uchezeshaji mbovu wa marefa, ambao tangu mwanzo walionekana kuwapendelea wenyeji.
Azam juzi walinyimwa penalti mbili za halali, moja kila kipindi, ya kwanza baada ya shuti la mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kuzuiwa kwa mkono na beki wa Shark na ya pili kiungo Humphrey Mieno aliangushwa kwenye eneo la hatari, tena ndani ya sita akiwa amekwishamtoka kipa, lakini zote refa akapeta.
Washika vibendera nao walizima mashambulizi kadhaa ya Azam kwa kudai wachezaji walikuwa wameotea.
Mabao yote Azam walifungwa wakitoka kushambulia na hayakuwa na mushkeli, makosa ambayo walirekebisha na hawakuyarudia kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza, timu zilishambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Azam walitawala zaidi mchezo na kama si ‘madudu’ ya refa, matokeo yangeweza kubadilika.
Azam ilicheza mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Watano hao, waliwasili mjini DRC jana na leo Azam inatarajiwa kushusha kikosi chake kamili. Beki Joackins Atudo naye anatarajiwa kuungana na timu leo mjini hapa.
Nusu Fainali zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.  Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa. 

0 comments:

Post a Comment