.

.
Friday, November 23, 2012

10:57 AM
Rais Kikwete akipiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa CCM uliofanyika Dodoma hivi karibuniNa Mwandishi wetu, Karagwe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kinafurahi kuona kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatekeleza sera walizozianzisha wao.
Kauli ya CHADEMA ilitolewa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, wakati akifungua rasmi Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kagera ambalo linaundwa na viongozi kutoka katika kila jimbo la mkoa huo, linalofanyika kwa muda wa siku tatu katika wilaya ya Karagwe.
Dk. Slaa alisema CHADEMA waliwezesha kufutwa kwa kodi za manyanyaso katika wilaya ya Karatu baada ya kulikalia kidete suala hilo, na ndipo CCM ilitumia sera hiyo na kuondoa kodi za namna hiyo takriban nchi nzima.
Aliongeza kuwa walianzisha pia sera ya kujenga zahanati kila kata wilayani Karatu, ambayo nayo CCM baadaye ilichukua na kisha kutangaza kuanzisha utaratibu wa kujenga zahanati kila kata nchi nzima.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2010, CHADEMA tuliahidi sera ya kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi nchi nzima kama tungeingia madarakani. Wakati huo CCM ilidai haiwezekani ila sasa nao wametangaza kupunguza gharama za bidhaa hizo,” alisema.
Alifafanua ni wazi kuwa CCM ikiweza kutekeleza sera ya CHADEMA ya kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na kutoa elimu bure kabla ya mwaka 2015, watafurahi maana hawana wivu, lakini wakishindwa itakuwa ndiyo njia yao ya kuondoka madarakani.
Dk. Slaa aliongeza kuwa CHADEMA haiwezi kuchukia kutokana na CCM kutekeleza sera zake maana zinapotekelezwa wananchi wanapata mabadiliko na unafuu wa maisha.
Alisema kuwa kelele zao zinahitaji uchumi wa nchi usimamiwe vizuri na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wote, na kwamba mpaka sasa inashangaza kuona CCM imeshindwa kupata majibu yanayosababisha wananchi kuendelea kuwa maskini.
Dk. Slaa alichanganua kuwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliweza kuanzisha viwanda ambavyo sasa vingi vimefungwa, bila kuchimba dhahabu na wala kuuza samaki nje ya nchi, lakini akahoji ni kwa nini wakati huu ambao tunauza madini, samaki nje ya nchi maendeleo yamedumaa.
“Mfano Waingereza hawana mashamba makubwa lakini hata siku moja hawakuwahi kulia njaa. Sisi Tanzania tuna mabonde makubwa ambayo yakitumiwa ipasavyo mawili yanaweza kutosha kulisha nchi nzima, lakini bado tunalia njaa,” alisema.
Alibainisha kuwa kutokana na kutokuwa na mpangilio mzuri, mawazo mgando yaliyopo hayawezi kuleta maendeleo. Alitolea mfano kuwa inashangaza kuona bado tuna treni inayosafiri siku tatu kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Katibu huyo aliwataka viongozi wa chama hicho kutoogopa kukemea maovu yanayofanywa na baadhi ya viongozi walioko madarakani na kwamba kiongozi bora lazima aonyeshe madadiliko katika eneo lake.
Alisema CHADEMA iko katika harakati za kuboresha na kuimarisha utendaji kazi wa ndani kwa kununua pikipiki kila kata nchi nzima, kuajiri makatibu na kutafuta ofisi za kudumu na zenye hadhi.

0 comments:

Post a Comment