.

.
Sunday, November 25, 2012

7:58 PM
Kikosi cha timu ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars kilichoifunga 2-0 Sudan leo Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge 2012. Kutoka kulia waliosimama ni Nahodha Juma Kaseja, Kevin Yondan, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe. Walioinama kutoka kushoto ni Salum Abubakar, Simon Msuva, Amir Maftah, Frank Domayo na Mrisho Ngassa.

John Bocco 'Adebayor' akigombea mpira na beki wa Sudan

Mashabiki Stars kwa raha zao

Wachezaji Stars wakimpongeza Bocco baada ya kufunga bao la kwanza

Benchi la Ufundi Stars, kutoka kushoto kocha Mkuu, Kim Poulsen, Msaidizi wake, Sylvester Marsh, Meneja, Leopold Tasso 'Mukebezi na kocha wa makipa Juma Pondamali

Waandishi wa Habarfi wa Tanzania waliokuja Kampala kutoka kulia Alex Luambano, Sostenes Nyoni, Timzo Kalugiwa, Somoe Ng'itu, Zaituni Kibwana wakiwa na rais wa CECAFA, Leodegar Tenga na Katibu wake, Nicholaus Musonye

Amir Maftah akimtoka beki wa Sudan

Erasto Nyoni akitafuta mbonu za kumtoka beki wa Sudan

Salum Abubakar akigombea mpira na kiungo wa Sudan

Simon Msuva akigombea mpira na beki wa Sudan

Mrisho Ngassa akimtoka beki wa Sudan

John Bocco aliingia nao mpira nyavuni kufunga bao la pili 
Wachezaji Stars wakimpongeza Bocco kushoto kwa kucheza sebene
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, imeanza vema kampeni zake za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, baada ya kuichapa mabao 2-0 Sudan katika mchezo uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda. 
Ushindi huo, unaiweza Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, nyuma ya Burundi inayoongoza kwa wastani wa mabao.
Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yote yakipachikwa kimiani na mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyetumia vema krosi za Mrisho Khalfan Ngassa.
Bocco alifunga bao la kwanza Bocco aliiwahi vema krosi ya Ngassa aliyewatoka mabeki wa Sudan wingi ya kushoto na kuitumbukiza kimiani dakika ya 14.
Adebayor wa Chamazi aliwainua tena vitini mashabiki wa Tanzania dakika ya 28, akiunganisha krosi ya Ngassa tena kutoka kule kule kushoto. 
Kwa ujumla Tanzania Bara walicheza vizuri kipindi cha kwanza, wakishambulia zaidi kupitia pembeni, kulia Simon Msuva ambaye hakuwa na madhara sana na kushoto Ngassa ambaye alikuwa mwiba mchungu haswa kwa Wasudan.
Pamoja na Bara kutawala kipindi cha kwanza, lakini Wasudan walifanya mashambulizi kadhaa ya kushitukiza na sifa zimuendee mlinda mlango Juma Kaseja, ambaye alioko amichomo miwili ya hatari mno. 
Kipindi cha pili Stars, inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen iliendelea kutawala mchezo, lakini safu ya ulinzi ya Sudan iligangamala.
Tanzania Bara; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar/Amri Kiemba, John Bocco, Mwinyi Kazimoto na Simon Msuva/Shaaban Nditi.
Sudan; Ebd Elrahman Ali, Moawia El Amin, Sami Abdallah, Faris Abdallah, Hamoda Bashir/Farid Mohamed, Mohamed El Mortada, Sadam Abutalib, Mohamed Mussa Idris, Modathir Mohamed, Adam Sayer/Osama El Rashid na Mohamed Osman/Saed Siddig.   
Katika mchezo wa awali, Burundi walishinda mabao 5-1, mabao yake yakifungwa na Chris Nduwarugira dakika ya 35 na 88, Yussuf Ndikumana dakika ya 41 na Suleiman Ndikumana dakika ya 84 na 90, wakati la Somalia lilifungwa na Mohamed Jabril kwa penalti dakika ya 55.
Matokeo hayo yanalifanya Kundi B lizidi kuwa gumu, kwani Burundi inaongoza kwa pointi zake tatu na mabao mengi, Tanzania ya pili kwa pointi tatu na mabao mawili- lakini bado Sudan wanaweza kupata matokeo mazuri katika mechi zijazo.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Injinia Leodegar Chillah Tenga (kushoto) akisalimiana  na Mjumbe wa Heshima wa CECAFA, Alhaj Muhiddin Ahmad Ndolanga kulia kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda kabla ya mechi ya Kundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na kati, CECAFA Tusker Challenge kati ya Tanzania Bara na Sudan jioni hii.
 
.........xxx................xxx............xxx...........

STARS YAANZA KAZI KAMPALA LEO USIKU

John Bocco 'Adebayor' ataongoza safu ya ushambuliaji Stars leo?

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
TIMU ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars leo inatarajiwa kuanza kampeni zake za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge leo itakapomenyana na Sudan kuanzia saa 12:00 jioni Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Mchezo huo, utatanguliwa na mchezo mwingine wa Kundi B kati ya Somalia na Burundi, kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja huo huo.
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesikitishwa na kutowasili kwa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaweza wasicheze katika mechi ya kwanza kwa sababu hawajafika, lakini mimi nikiwa kocha nimejiandaa vizuri na nina imani na wachezaji waliopo,” alisema.
“Nina imani TFF wanafuatilia suala hili na wachezaji hawa watajiunga na wenzao hivi karibuni lakini hii haituzuii kufanya vizuri kwani tumejiandaa vizuri,” alisema.
Alisema wachezaji wote wana hali nzuri na wana ari ya kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Sudan ambazi zimo katika Kundi B pamoja na Burundi na Somalia ambazo zitacheza leo pia.
Hata hivyo, jana Kili Stars walilalamikia Uwanja mbovu wa Chuo Kikuu cha Kampala Kampasi ya Biashara, waliopelekwa kufanya mazoezi kujiandaa na mechi ya leo.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura aliwasilisha malalamiko hayo kwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Rodgers Mulindwa ambaye ameahidi kuyafanyia kazi.
“Tutalifanyia kazi suala hilo, tutakuwa na kikao kesho (leo) litawasilishwa na litapatiwa usumbufu, mwanzo huwa na matatizo, lakini mambo yatakuwa mazuri,”alisema Mulindwa.
Hata hivyo, inashangaza Stars kupelekwa katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Kampala Kampasi ya Biashara, wakati kwenye mpango wa awali kabisa wa FUFA ilitakiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nakawa.    

0 comments:

Post a Comment