.

.
Thursday, November 8, 2012

9:44 AM

Serikali imeamua kuwavalia njuga watu wote wanaowanyanyasa watoto wa kike na kuwanyima haki zao za msingi hasa ya elimu kwa kigezo cha mila na desturi zisizo na tija wala manufaa kwa Taifa.





Akiongea na kipindi hiki wilayani ngorongoro, mkuu wa wilaya ya hiyo mheshimiwa Elias Wawa Lali amesema kuwa kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya watu hasa wa jamii ya kimasai kuwakatisha watoto wao masomo na kuwalazimisha kuolewa kwa kigezo cha mila na desturi ambapo kuanzia sasa watu hao ameanza kuwachukulia hatua kali za kisheria.





Alisema kuwa jamii hiyo ya kimasai wamekuwa wakiwachukulia watoto wa kike kama chombo cha biashara au starehe hali ambayo imekuwa chanzo cha kushuka kwa taaluma wilayani humo kutokana na watoto hao kukatishwa masomo au kulazimishwa kujifelisha mitihani ya darasa la nne au la saba ili kuolewa na wakikaidi hutishiwa kuachiwa laana.





Millya aliongeza kuwa kumkatisha mtoto masomo kwa ajili ya kupata ng’ombe kwa jamii hiyo imekuwa kama kawaida kwa jamii hiyo hali ambayo serikali haikubaliani nalo kwani ni kinyume na sera ya nchi ya kumuelimisha mtoto wa kike hivyo wameanza kuwachukulia hatua kali kali za kisheria wahusika wa vitendo hivyo ambapo pia amewataka watoto au wasamaria wema waonapo vitendo hivyo kwa majirani zao watoe taarifa mapema.





Aliongeza kuwa awali walikuwa wakitoa elimu juu ya madhara ya kuendekeza mila na desturi hasa kwa mtoto wa kike ambao ndio waathirika wakubwa na mila hizo lakini wako baadhi ya wananchi wanaojifanya mawazo yao hayabadiliki hivyo sasa wameamua kuwachukulia hatua za kisheria.





Awali uchukuzi uliofanywa na kipindi hiki wilayani humo umebaini kuwa swala la mila na desturi katika jamii hiyo ya kimasai bado ni Mungu mtu lakini utekelezaji wake humkandamiza zaidi mtoto wa kike hasa katika umri wa miaka 10 na kuendelea ambapo hulazimishwa kukeketwa sambamba na  kulazimishwa kuolewa na mtu hata asiyemtaka kwa kigezo cha wazazi kupewa mali au ngombe bila kujali umri wala masomo yake.

0 comments:

Post a Comment