.

.
Monday, November 26, 2012

8:04 PM
Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha
Watu watatu kati ya watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa baada ya kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi. Tukio hilo lilitokea jana muda wa saa 3:45 asubuhi katika eneo la olmatejoo lililopo jijini Arusha.
Akithibitisha taarifa hizo ofisini kwake jana mchana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas alisema kwamba, walipata taarifa toka kwa raia wema juu ya uwepo wa watu watano waliokuwa wanatiliwa shaka katika eneo la olmatejoo.
Kamanda Sabas aliongeza kwa kusema kuwa, mara baada ya kupata taarifa hiyo, baadhi ya askari waliokwenda katika eneo hilo kwa nia ya kufanya uchunguzi, lakini watu hao walishtuka na mmoja wao alichomoa bastola kiunoni na kuanza kuwafyatulia risasi askari hao.
Kufuatia hali hiyo askari hao waliamua kujibu mapigo na kufanikiwa kuwajeruhi watu watatu ambao walichukuliwa na kupelekwa hospitali huku wengine wawili akiwemo aliyekuwa na bastola wakifanikiwa kukimbia. Wakiwa njiani kwenda hospitali ya Mount Meru watu hao walifariki dunia.
“Mara baada ya mapambano ya kurushiana risasi askari walifanikiwa kupata begi la watu hao na baada ya kulipekua walikuta bunduki mbili; moja aina ya Shortgun na nyingine aina ya Rifle yenye namba 08805 ambayo ilikuwa imekatwa kitako pamoja na mtutu, risasi 16 za shortgun, kipande cha chuma (mtalimbo) ambacho kinasadikiwa kutumika katika uvunjaji.” Alifafanua Kamanda Sabas
Mbali na orodha hiyo pia begi hilo lilikutwa na rungu, panga, tupa tatu za kunololea, kofia mbili zinazotumika kuficha uso na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambazo ni kofia moja, suruali moja na T-shirt moja. Pia askari hao walifakiwa kupata kitambulisho cha kura na kitambulisho cha Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Dodoma pamoja na leseni ya udereva ambavyo wamiliki wake bado hawajapatikana.
Mpaka hivi sasa majina ya watu hao ambao ni wanaume bado hayajajulikana na Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na juhudi za kutafuta majina yao. Pia Jeshi hilo linaendelea kuwasaka watu wengine wawili ambao walifanikiwa kukimbia. Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru.
Kamishna huyo Msaidizi wa Polisi alimalizia kwa kutoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Pia alionya kwa kusema kwamba, watu wanaofikiria kufanya uhalifu katika kipindi cha kuelekea mwisho wa Mwaka waondoe kabisa mawazo hayo kwani Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha lipo imara kila kona.

0 comments:

Post a Comment