.

.
Friday, November 23, 2012

11:23 AM
Di Matteo amebaki historia Chelsea

BILIONEA Mrusi Roman Abramovich amemfukuza kazi Kocha Mtaliano, Roberto Di Matteo asubuhi ya leo baada ya matokeo mabaya mfululizo.
Mmiliki huyo wa Chelsea, amekasirishwa na matokeo mabaya ya timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, na kumfukuza kazi Mtaliano huyo baada ya timu kuzabwa mabao 3-0 na Juventus jana, ikiwa ni miezi sita tu tangu aipe timu hiyo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Sasa mtu wa kwanza kabisa ambaye Abramovich anamtaka akarithi mikoba ya Mtaliano huyo ni kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, na kama akikwama kwa Mspanyola huyo ambaye amesema hataki ukocha tena kwa sasa, basi atahamishia ndoana zake kwa Rafa Benitez.
MAKOCHA WALIODUMU MUDA MFUPI CHESLEA:
Guus Hiddink         Siku 105
Felipe Scolari         Siku 223
Avram Grand          Siku 247
Andre Villas-Boas   Siku 256
Roberto Di Matteo   Siku 262
MATOKEO YALIYOMFUKUZISHA KAZI DI MATTEO:
Oktoba 23: Shakhtar 2 Chelsea 1        (Ligi ya Mabingwa)
Oktoba 28: Chelsea 2 Man United 3    (Ligi Kuu)
Oktoba 31: Chelsea 5 Man United 4    (Kombe la Ligi)
Novemba 3: Swansea 1 Chelsea 1      (Ligi Kuu)
Novemba 7: Chelsea 3 Shakhtar 2      (Ligi ya Mabingwa)
Novemba 11: Chelsea 1 Liverpool 1     (Ligi Kuu)
Novemba 17: West Brom 2 Chelsea 1  (Ligi Kuu)
Novemba 20: Juventus 3 Chelsea 0     (Ligi ya Mabingwa)

                 ...................xxx............xxx..................xxx............... 

SUNZU KUENDELEA KUOGELEA KWENYE FWEZA MSIMBAZI

Feliux Sunzu akitibiwa

Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. ataongezewa mkataba baada ya kumaliza mkataba wake wa awali mwishoni mwa msimu katika klabu ya bingwa Tanzania Bara, Simba SC.
Kiongozi mmoja wa Simba amesema jana kwamba klabu hiyo imeridhika na huduma ya mchezaji huyo mrefu na inahitaji kuendelea naye.  
Kumekuwa na mawazo tofauti ndani ya Simba SC kuhusu Sunzu, ambaye kwa sasa ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi Tanzania, Sh Milioni 5, kwamba hachezi kwa kiwango cha fedha anazolipwa.
Lakini wengine wanaamini Sunzu anawajibika vizuri na anastahili kwa fedha anayolipwa. Pamoja na hayo, hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo kwa sasa, inatia shaka kama itaweza kuurudia mkataba ule ule wa Sunzu.
Hata hivyo, habari zaidi zinasema kwamba Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameamua kumaliza suala la Sunzu kwa kumsainisha mkataba mpya hivi karibuni.
Baada ya kumaliza mkataba wa awali, Simba ili kuendelea kuishi na Sunzu, inakadiriwa kumpa fedha ya dau la usajili, ambalo kwa mwaka haliwezi kuwa chini ya dola za Kimarekani 15,000 (zaidi ya Sh. Milioni 20 za Tanzania) na kukubaliana kuhusu mshahara uwe ule ule au mpya.
Kulingana zengwe lililotawala juu ya dola za Kimarekani 3,500 anazolipwa Sunzu kuna uwezekano Simba ikataka kuuteremsha mshahara huo, lakini habari zilizopatikana jana zimesema kwamba Sunzu ataendelea kulipwa mshahara ule ule katika mkataba wake mpya.
Kumalizika kwa mkataba wa Sunzu ni mtihani mwingine kwa Simba, ambayo kwa sasa inakabiliwa na kasheshe la kuingia mkataba mpya na mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi ambaye yuko vizuri kisoka na anatolewa macho na Azam na Yanga.
Na suala la usajili linaonekana kuwa zito kwa wakati huu, kwa sababu Kamati ya Utendaji ya Simba SC wiki hii imevunja Kamati zote ndogondogo, ikiwemo Kamati ya Usajili, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Zacharia Hans Poppe.   
Hata hivyo, inadaiwa vibopa wa Kamati ya Usajili, akiwemo Hans Poppe watarejeshewa majukumu hayo. 
             ................xxx......................xxx..........................xxx

MASHABIKI KANDA YA ZIWA WAENDA KUISAPOTI STARS KAMPALA


Frank Domayo, kiungo wa Kili Stars

Na Mahmoud Zubeiry
UMOJA wa wanamichezo waliowahi kucheza klabu mbalimbali zikiwemo za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara wenye maskani yao mjini Bukoba, Kagera, Bukoba Veteran Sports Club ni katika kuhamasisha ushiriki wa timu za Tanzania, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes, kwenye michuano ya Kombe la Tusker Challenge inayofanyika jijini Kampala Uganda, umeandaa safari ya mashabiki walioko mkoani humo Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwenda kushangilia mechi za timu hizo.
Katibu Mkuu wa Bukoba Veterans, Shijja Richard ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba kwa kuanzia, mashabiki hao wataondoka mjini Bukoba Jumapili Novemba 25, 2012 kwenda kuishangilia timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Sudan Kaskazini.
Amesema nia na madhumuni ya safari hiyo ni kuhamasisha wachezaji wa timu za taifa za Tanzania waweze kufanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kutoa hamasa kwa watanzania kujenga tabia ya kushangilia timu zao na pia wanadhani kuwa ushiriki wao utaongeza ushindani katika michuano hiyo.
Amesema tayari taratibu zote zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ili wawasiliane na mamlaka zinazohusika kwa ajili ya kupatiwa eneo maalumu uwanjani litakalowezesha watanzania waweze kuishangilia vizuri timu ya taifa.
“Tunatarajia kwenda uwanjani na zaidi ya mashabiki 60 ambao hivi sasa wanakamilisha taratibu za mwisho za kuvuka mpaka wa nchi. Matarajio yetu ni kuendelea kuziunga mkono timu za taifa katika michuano hiyo hadi kufikia mwisho wa michuano. Tunaomba watanzania wengine walioko kanda ya ziwa katika mikoa ya Shinyanga, Mara na Mwanza watuunge mkono,”alisema Richard.
Kikosi cha kinatarajiwa kuwasili leo mjini Kampala, kikitokea Mwanza tayari kwa mashindano hayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Tusker Challenge 2012 yanayotarajiwa kuanza kesho.
Stars imekuwa kambini mjini Mwanza kwa takriban wiki mbili sasa ikijifua vikali chini ya kocha wake, Mdenmark Kim Poulsen kujiandaa kwenda kutwaa taji la nne la Challenge.
Kikosi cha Kilimanjaro Stars kilichopo kambini mjini Mwanza, kinaundwa na makipa; Juma Kaseja (Simba SC) na Deogratius Mushi ‘Dida’ wa Azam FC, mabeki; Kevin Yondan (Yanga), Erasto Nyoni (Azam FC), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Shomari Kapombe na Amir Maftah (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa (Simba), Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo (Yanga) na Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar) wakati washambuliaji ni John Bocco ‘Adebayor’ (Azam FC), Simon Msuva (Yanga), Christopher Edward (Simba), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa (TPM, DRC).
Bara ambayo inajivunia kutwaa mara tatu Kombe la Challenge katika miaka ya 1974, 1994 na 2010 na kushika nafasi ya pili mara tano, imepangwa Kundi B pamoja na Sudan, Burundi na Somalia.
Itaanza kampeni zake Novemba 25 kwa kumenyana na Sudan saa 12:00 jioni, mchezo utakaotanguliwa na mechi kati ya Burundi na Somalia itakayoanza saa 9:00 Alasiri kabla ya kurudi tena dimbani, Novemba 28 kukipiga na Burundi, mchezo utakaotanguliwa na mechi kati ya Somalia na Sudan.
Stars iatahitimisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na Somalia Desemba 1, mchezo utakaotanguliwa na mechi nyingine kati ya Sudan na Burundi. Mechi zote za Stars zitakuwa saa 12:00 jioni.
MAKUNDI RATIBA TUSKER CHALLENGE 2012:
KUNDI A: Uganda, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini
KUNDI B: Tanzania, Sudan, Burundi na Somalia
KUNDI C: Malawi, Eritrea, Rwanda na Zanzibar
RATIB KUNDI A:
Novemba 24, 2012:
Ethiopia v Sudan                 (Saa 9:00 Alasiri)
Uganda v Kenya                  (Saa 12:00 jioni)
Novemba 27, 2012:
Sudan Kusini v Kenya         (Saa 9:00 Alasiri)
Uganda v Ethiopia              (Saa 12:00 jioni)
Novemba 30, 2012:
Kenya v Ethiopia                 (Saa 9:00 Alasiri)
Sudan Kusini v Uganda      (Saa 12:00 jioni)
RATIBA KUNDI B:
Novemba 25, 2012:
Burundi v Somalia               (Saa 9:00 Alasiri)
Tanzania v Sudan                (Saa 12:00 jioni)
Novemba 28, 2012:
Somalia v Sudan                  (Saa 9:00 Alasiri)
Tanzania v Burundi             (Saa 12:00 jioni)
Desemba 1, 2012:
Sudan v Burundi                  (Saa 9:00 Alasiri)
Somalia v Tanzania             (Saa 12:00 jioni)
RATIBA KUNDI C:
Novemba 26, 2012:
Zanzibar v Eritrea         (Saa 9:00 Alasiri)
Rwanda v Malawi         (Saa 12:00 jioni)
Novemba 29, 2012:
Malawi v Eritrea                  (Saa 9:00 Alasiri)
Rwanda v Zanzibar             (Saa 12:00 jioni)
Desemba 1, 2012:
Malawi v Zanzibar               (Saa 9:00 Alasiri)
Eritrea v Rwanda                 (Saa 12:00 jioni)
ROBO FAINALI:
Desemba 3, 2012
Mshindi Kundi C vs Mshindi wa Pili Kundi B (Saa 10:00 jioni)
Mshindi Kundi A vs Mshindi wa Tatu Bora wa pili (Saa 1:00 usiku)
Desemba 4, 2012 (16:00):
Mshindi Kundi B vs Mshindi wa Tatu Bora wa kwanza (Saa 10:00 jioni)
Mshindi wa Pili Kundi A vs Mshindi wa Pili Kundi C    (Saa 1:00 usiku)
NUSU FAINALI:
Desemba 6, 2012
Nusu Fainali ya Kwanza     (Saa 10:00 jioni)
Nusu Fainali ya Pili              (Saa 1:00 usiku)
MSHINDI WA TATU:
Desemba 8, 2012
Waliofungwa Nusu Fanali (Saa 10:00 jioni)
FAINALI:
Desemba 8, 2012
Walioshinda Nusu Fainali  (Saa 1:00 usiku)

na Bin Zubery blog

0 comments:

Post a Comment