.

.
Monday, November 26, 2012

8:18 PM

YANGA KWENDA UTURIKI KUPIGA KAMBI YA WIKI MBILI, BRANDS APANDISHA MAKINDA MATATU YA  B  YANGA  A.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam leo. Kulia ni Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mholanzi, Ernie Brandts. Picha na Princess Asia

Na Princess Asia
KATIKA kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga ya Dar es Salaam inatarajia kwenda kuweka kambi ya wiki mbili nchini Uturuki mapema mwakani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kwamba ziara hiyo inatarajiwa kufanyika kati ya Desemba na  Februari 25, mwakani.
Alisema pendekezo la kambi hiyo lilitolewa na kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts ambaye ana uzoefu na nchi hiyo ambayo ina vitu vinavyostahili kwa ajili ya timu kuweka kambi.
Alisema ikiwa huko timu hiyo inatarajiwa kucheza mechi mbili za kitrafiki na timu zitkazotajwa baadaye.
Aidha, kocha mkuu wa timu hiyo amewapandisha wachezaji watatu wa kikosi cha vijana chini ya miaka 20 wakiwemo kipa, Yussuf Abdallah, George Banda na Rehan Kibinga.
Katika hatua nyingine, Bin Kleb aliasema wanajivunia uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Manji, kwani timu imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame, kufanya vema katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ambao ulimalizika kwa timu kuongoza.
Alisema kufanya vizuri katika Ligi Kuu, ni matunda ya timu hiyo kuweka kambi nchini Rwanda baada ya Kombe la Kagame.

BOCCO ANAVYOTISHA KAMPALA, BADO WASOMALI NA WARUNDI WATAMKOMA

John Raphael Bocco 'Adebayor', atatwaa kiatu cha dhahabu CECAFA Tusker Challenge 2012?

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
JOHN Bocco ‘Adebayor’ ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanaowania ufungaji bora wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kufuatia jana kufunga mabao mawili, Tanzania Bara ikiilaza Sudan 2-0 katika mchezo wa Kundi B, Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda.
Bocco aliyeifungia Kilimanjaro Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager mabao yote hayo kipindi cha kwanza, sasa analingana na washambuliaji wa Burundi, Chris Nduwarugira na Suleiman Ndikumana, ambao kila mmoja ana mabao mawili pia.
Wengine ambao hadi sasa kila mmoja amefunga bao moja ni Yussuf Ndikumana wa Burundi, Mohamed Jabril wa Somalia kwa penalti, Geoffrey Kizito wa Uganda na Yonatal Kebede Teklemariam.
Bocco ana nafasi zaidi ya kuongeza mabao katika mechi za kundi hilo, haswa kwenye mchezo dhidi ya Somalia Desemba 1, kwani hiyo ndio timu dhaifu zaidi kwenye Kundi B.
Lakini Bocco kama atacheza kwa kiwango cha jana, anaweza akawa mwiba hata mbele ya Burundi Novemba 28.
Kwa sasa Bocco anayechezea Azam FC ya Dar es Salaam, ndiye mshambuliaji pekee kwenye kikosi cha Bara, baada ya washambuliaji wengine, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemomkrasia ya Kongo (DRC) kuzuiliwa na klabu yao.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
John Bocco                  Tanzania 2
Yussuf Ndikumana       Burundi   2
Suleiman Ndikumana   Burundi   2
Yussuf Ndikumana       Burundi   1
Mohamed Jabril            Somalia   1(penalti).
Geoffrey Kizito              Uganda    1
Yonatal Teklemariam    Ethiopia   1
 
                 .............XXX................XXX.................XXX..............

NGASSA ATETEMESHA KAMPALA BALAA, WAGANDA TUMBO JOTO

Ngassa alivyokuwa akiteleza kushoto mwa uwanja wa namboole jana, balaa

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
SALUTI kwa Mrisho Khalfan Ngassa. Waganda, wamekoma naye. Mashabiki wa soka Uganda, wamekoshwa na soka ya Mrisho Khalfan Ngassa wa Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge inayoendelea mjini hapa.
Wakizugumza baada ya mechi kati ya Sudan na Tanzania, mashabiki walikuwa wakimsifia mno mchezaji huyo wa Tanzania Bara aliyekuwa amevalia jezi namba nane na kusema hawajui siku Stars ikikutana na Uganda itakuwaje mbele ya mshambuliaji huyo wa Simba SC ya Dar es Salaam.
Hata Waandishi wa Habari wa Uganda, wamemsifia mno Ngassa wakisema huyo ndiye mchezaji aliyeonyesha kiwango kikubwa zaidi cha uchezaji hadi sasa kwenye michuano hii.
Ngassa jana alikuwa mwiba kweli mbele ya Sudan, akitengeneza mabao yote mawili ya ushindi yaliyofungwa na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC.
Jana Ngassa alipangwa wingi ya kushoto ambako alikuwa akiteleza kwa kasi na kutoa krosi nzuri ambazo bahati mbaya au nzuri ni mbili tu zilizotumiwa vyema na Bocco.
Mashabiki wamemsifia pia Ngassa kwamba si mchezaji mchoyo ambaye muda wote anafikiria zaidi kuwatengenezea wenzake nafasi kuliko kutaka kufunga mwenyewe.
Ngassa ni kati ya wachezaji 10 wa Simba wanaocheza michuano ya mwaka huu mjini hapa, wengine wakiwa ni Nassor Masoud 'Cholo' (Zanzibar), Juma Kaseja (Bara), Shomari Kapombe (Bara) Amir Maftah (Bara), Amri Kiemba, (Bara) Mwinyi Kazimoto (Bara), Ramadhani Singano ‘Messi’ (Bara), Christopher Edward (Bara) na Emanuel Okwi (Uganda).
Timu nyingine za Bara zenye wachezaji hapa ni Azam tisa, Mwadini Ali (Zanzibar), Abdulaghan Gulam (Zanzibar ), Samir Haji Nuhu(Zanzibar), Aggrey Morris(Zanzibar), Khamis Mcha 'Vialli'(Zanzibar), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Bara), Erasto Nyoni (Bara), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Bara) na John Bocco ‘Adebayor’ (Bara).
Yanga ina wachezaji saba, ambao ni Nadir Haroub Ali 'Canavaro'(Zanzibar), Haruna Niyonzima (Rwanda), Hamisi Kiiza (Uganda), Kevin Yondan (Bara), Athuman Iddi ‘Chuji’ (Bara), Frank Domayo (Bara) na Simon Msuva (Bara), wakati Mtibwa Sugar inao watatu Twaha Mohammed (Zanzibar), Issa Rashid (Bara) na Shaaban Nditi (Bara), JKT Oljoro ina mmoja Amir Hamad (Zanzibar) sawa na Coastal Union Suleiman Kassim 'Selembe' wa  Zanzibar pia. 

ZANZIBAR HEROES WAANZA KAZI LEO KAMPALA

Zanzibar Heroes watang'ara leo?

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
TIMU ya soka ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes leo inaanza kampeni zake za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwa kumenyana na Eritrea katika mchezo wa Kundi C, utakaonza saa 9:00 alasiri Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa
Mchezo huo, utafuatiwa na mchezo mwingine wa kundi hilo, ambao unatarajiwa kuwa mkali zaidi na wa kusisimua kati ya Rwanda na Malawi kuanzia saa saa 12:00 jioni.
Kikosi cha Zanzibar Heroes kiliagwa Jumatano visiwani Zanzibar katika Hoteli ya Bwawani ambayo inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk.
Kikosi kiliondoka Alhamisi Zanzibar kuaa Kampala kikipitia Dares Salaam na kimeondoka na msafara wa watu 30, wakiwemo wachezaji 20, benchi la ufundi na viongozi wa Serikali na Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA).
Hata hivyo, Heroes itamkosa kiungo wake mahiri Abdulhalim Humud, ambaye ni majeruhi.
Kikosi kinachotarajiwa kuanza leo Heroes ni; Mwadin Ali Mwadini, Nassor Masoud ‘Cholo’, Samir Hajji Nuhu, Agrey Moris, Nadir Haroub Ali 'Canavaro, Sabri Ali, Khamis Mcha 'Vialli', Is-haka Othman, Amir Hamad, Twaha Mohammed na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Tayari mechi za awali za Kundi A na B zimekwishachezwa na leo Kundi C ndio linafichua makali yake kwa mara ya kwanza.
Katika mechi za ufunguzi za Kundi A, Ethiopia waliifunga Sudan Kusini 1-0, wakati Uganda waliichapa Kenya 1-0 pia juzi, Uwanja wa Mandela, Namboole.
Mechi za Kundi B jana, Burundi iliitandika Somalia mabao 5-1, kabla ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kuilaza Sudan 2-0.  

0 comments:

Post a Comment