.

.
Monday, November 5, 2012

8:44 PM

KUKITHIRI kwa shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo kwenye mto Ruvu, kunahatarisha usalama wa viumbe hai waliopo mtoni ambao ni tegemeo kubwa la chanzo cha maji kwa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wachimbaji hao wakichimba dhahabu pembezoni mwa mto huo na kuacha mashimo makubwa, ambayo baadaye maji hutiririka kwenye mashimo na kusababisha athari za mazingira.
Omari Juma, ambaye ni mchimbaji mdogo alisema wamekuwa wakifanya shughuli hiyo kujipatia kipato na kwamba, hupata kati ya gramu tatu hadi 10 kwa siku.
Alisema wanauza gramu moja kwa Sh70,000, lakini hali ya soko bado siyo ya kuridhisha kwani iwapo kungekuwa na kituo maalumu wangeweza kuuza bei nzuri.



Naye Thomas Laurence alisema upatikanaji dhahabu bado siyo nzuri, kwani wamekuwa wakipata kwa kubahatisha kutokana na kutokuwa na vifaa bora vya kuchimbia, lakini wanafanya shughuli hiyo kwa ajili ya kupata fedha ya kujikimu.



Hata hivyo, Laurence aliomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwawezesha kupata soko la uhakika la dhahabu yao na kuongeza kuwa, wachuuzi wa dhahabu hiyo wamekuwa wakinunua kwa bei ndogo.
Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro, Philip Ngeleja alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kwamba wachimbaji hao wanafanya shughuli hiyo kinyume cha sheria ya madini ya mwaka 2010.
“Uchimbaji wa madini lazima ufanyike chini ya leseni halali na kwamba, mtu atakayepatikana na hatia ya kuchimba bila leseni atatozwa faini isiyozidi Sh5 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu jela au vyote viwili kwa pamoja, kama ni kampuni itatozwa faini isiyozidi Sh50 milioni na kutaifishwa madini yote yaliyochimbwa ikiwamo mali zote za kampuni husika,”alisema Ngeleja.
Pia, Ngeleja alisema shughuli za uchimbaji madini zinafanyika hasa wakati wa kiangazi, wakati kina cha maji hupungua hivyo dhahabu iliyosombwa na maji kutoka milimani hupatikana kwa urahisi.
Hata hivyo, Ngeleja alisema jitihada zinafanywa na ofisi ya madini mkoa kwa kushirikiana na ofisi ya Bonde Wami Ruvu, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na wadau wengine wakiwamo viongozi wa vijiji, kata na tarafa kudhibiti uchimbaji huo ili kuepusha athari za mazingira.



Ofisa Maji Bonde la Wami Ruvu, Praxeda Karugendo alisema sheria na sera ya rasilimali za maji ipo wazi kwa watu kutofanya shughuli yoyote mita 100 kandokando ya mto na kwamba, wanatakiwa kutambulika kisheria na mamlaka husika.
Karugendo alisema wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na wadu mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo.



Kwa upande wake, Mtendaji Kijiji cha Kibangile, Aclay Paschael alielekeza shutuma kwa vyombo vya dola kushindwa kudhibiti tatizo hilo, kwani viongozi wa kijiji hadi tarafa wamekuwa wakifanya jitihada za kuwakamata watu hao lakini Polisi Kituo cha Matombo huwaachia saa chache baada ya kukamatwa.
“Tunashindwa kuelewa, watu wanakamatwa lakini wanaachiwa wakati sheria zipo wazi na hivi karibuni tumemkamata mchimbaji mmoja, akatozwa Sh400,000 baadaye kaachiwa kama angefungwa mtu mmoja ingekuwa fundisho,”alisema Paschael.
chanzo cha habri: gazeti la mwananchi 

0 comments:

Post a Comment