.

.
Sunday, November 11, 2012

3:08 AM



 
BAADHI ya wafungwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wanadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa Polisi kuwatoa kwa nguvu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwenye nyumba walizokuwa wakiishi katika Kambi Kuu ya mjini Moshi.

Tofauti na ilivyozoeleka ambapo hushuhudiwa FFU wakitumika kusambaratisha mikusanyiko ya watu wenye lengo la kuhatarisha amani, askari hao walitolewa kwa nguvu kwenye nyumba hizo na wafungwa hao ambao wanadaiwa kutoa vyombo vyao nje.

Tukio hilo lililowaacha vinywa wazi watu wengi mkoani Kilimanjaro, limewapata FFU waliokuwa wakiishi kwenye nyumba tatu zilizopo katika kambi kuu ya polisi mjini Moshi.

Taarifa zinadai FFU hao ilibainika kuwa   hawakupaswa kuishi katika nyumba hizo, badala yake polisi wa kawaida ndio waliopaswa kuishi, hivyo waliondolewa ili polisi hao waingie.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alipoulizwa na gazeti hili alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema: “Hayo ni masuala ya ndani ya polisi, siyo ya kuyaandika.”

Habari zaidi zinapasha kuwa tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita zikieleza kuwa kigogo mmoja wa polisi (jina tunalo), ndiye aliyewatumia wafungwa hao kuvamia na kuvunja milango ya nyumba za FFU hao ili kuwaondoa kwa nguvu, akidai kuwa alitumia njia za busara kuwataka watoke lakini walionekana  kuleta kiburi na kwamba hakuona sababu ya kuwatumia polisi.



“Ilikuwa saa 5:00 asubuhi ndipo alikuja bosi wetu (jina tunalihifadhi) akiwa na wafungwa, wakavunja milango ya nyumba za hao jamaa (FFU) na kutupa vyombo vyao nje,” kilieleza chanzo chetu.


Habari zaidi zimedai kuwa kigogo huyo mwenye cheo kikubwa alitumia mbinu hiyo kuwadhalilisha askari hao jambo linaloelezwa kuwasononesha FFU hao, huku polisi wengine wakipoteza morali wa kufanya kazi.
“Tuna mahakama zetu za kijeshi, kwa nini asitumie utaratibu huo kama hawakuingia kihalali waamriwe kutoa vitu vyao nje kwa njia ya kistaarabu badala ya kuwadhalilisha hivyo?” alihoji askari mmoja aliyeomba asiandikwe jina lake  kwa sababu za usalama.
Askari mwingine alisema kuwa kitendo cha kutupa vitu nje ya nyumba kwa kuwatumia wafungwa ni kuwadhalilisha polisi.


Alisema kuwa utaratibu uliozoeleka kambini hapo ni kwamba, polisi akitaka kuhama, aliye na shida ya nyumba ndiye anazungumza naye, ili kuangalia kama anaweza kumwachia nyumba husika au la.
chanzo cha habari; mwananchi


0 comments:

Post a Comment