.

.
Wednesday, November 7, 2012

10:21 AM
Vijana kote nchini wametakiwa kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa kujenga mazoea ya kuhudhuria semina na warsha mbali mbali za kimaendeleo zitakazowasaidia kujiajiri wenyewe kiujasiriamali kuliko kuendekeza kuhudhuria sehemu za starehe zisizo na tija kwao

mkufunzi katika mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana, bwana Bill Mushi akiwafundisha vijana somo la ujasiriamali (hawapo pichani
Rai hiyo imetolewa mkoani Arusha na mkufunzi katika  semina ya ujasiriamali  bwana Bill Mushi alipokuwa akiwafundisha vijana kutoka chuo cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha (AJTC) pamoja na vijana wengine kutoka sehemu mbalimbali mkoani hapa.

Mushi alisema kuwa kwa sasa duniani kote kuna tatizo la ajira, lakini tatizo hilo linakuzwa na vijana wenyewe kwa kutopenda kujikwamua kwa kujishughulisha na shughuli za kimaendeleo badala yake hubaki wakilalama  kuwa hakuna ajira huku kila siku kuna warsha na semina mbalimbali za kiujasiriamali lakini hawaudhurii badala yake utawakuta sehemu mbalimbali za starehe.

Kufuatia hali hiyo amewataka vijana kupambana na swala la tatizo la ajira wenyewe badala ya kubaki kulalamikia serikali kila kukicha huku wakiudhuria sehem za starehe zisizo na tija wala manufaa kwao wala kwa familia zao.
Pia aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kujaribu biashara mbalimbali ili kuweza kumudu soko la jumuiya ya Afika mashariki badala ya kubaki nyuma na kuwaachia wenzetu wa nchi jirani kama Kenya kutawala soko hilo kwani woga pia hufifisha maendeleo na kubaki kutafuta kazi za kuajiriwa badala ya kutafuta namna ya kujiajiri.

Kuanzia kushoto ni Mratibu wa semina hiyo ya ujasiriamali kwa vijana kutoka shirika la ajira duniani (ILO), Bwana Stanley E. Alphonce anayefuata ni mkurugenzi wa chuo cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha (AJTC) Bwana Joseph Mayagila na mwingine ni mratibu mshiriki wa semina hiyo ambaye pia ni mwalimu wa Chuo cha AJTC mwalim Andrea Ngobole wakisikiliza kwa makini mafunzo hayo ya ujsiriamali
Kwa upande wake mratibu wa semina hiyo kutoka shirika la ajira duniani, Stanley Alphonce alisema kuwa shirika limeamua kuandaa  semina hiyo kwa lengo la  kuwawezesha vijana kukabiliana na changamoto kubwa la ajira lililoko dunia nzima kwa sasa.

Alisema kuwa shirika la ajira duniani linaandaa semina mbali mbali za kuwasaidia vijana kuweza kujiajiri wenyewe kwa kuwapa mafunzo na mawazo ya kuweza kubuni shughuli za kiujasiriamali wenyewe sambamba na kuendesha biashara zao zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Naye mkurugenzi wa chuo cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha (AJTC), Bwana Joseph Mayagila akiongelea mafunzo hayo alisema kuwa yatawasaidia wanafunzi wao kujitambua katika mazingira ya kiuchumi, nafasi zao katika kukuza uchumi sambamba na changamoto za kimaisha pindi wakiwa bado shuleni pamoja na kuweza kujiajiri wenyewe wamalizapo chuo kuliko kutegemea kuajiriwa ambapo wakikosa wengi wao hukata tamaa ya maisha.

Baadhi ya wanafunzi wa wa chuo cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha (AJTC) kilichoko mbauda mkoani Arusha nchini Tanzania wakisikiliza kwa makini mafunzo ya ujasiriamali wanayopatiwa ili kuweza kujiajiri wenyewe kuliko kumaliza shule na kutegemea kuajiriwa
       vijana hao zaidi ya 200 wamefanikiwa kuhudhuria mafunzo hayo ya ujasiriamali ambapo pamoja na elimu ya uandishi wa habari na utangazaji pia wamepata mafunzo ya ujasiriamali na kubahatika kupatiwa vyeti hivyo sasa ni wajibu wao kuitumia elimu hiyo kwa manufaa au kwa hasara.......                                     

0 comments:

Post a Comment