.

.
Sunday, October 28, 2012

3:16 PM

UCHAGUZI  mdogo wa udiwani katika kata ya Darajambili Mkoani Arusha leo umeingia dosari baada ya risasi kurindima hewani mfulululizo asubuhi ya leo karibu na maeneo ya kupigia kura hali iliyozua taharuki kwa wakazi wa kata hiyo waliokuwa wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura.





Risasi hizo zinadaiwa kupigwa na mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki,Joshua Nassari pamoja na mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM(Uvccm) wilayani Arusha,Godfrey Mwalusamba mara baada ya kuibuka tafrani baina ya wafuasi wa CCM na Chadema katika eneo la Shule ya sekondari ya Felix Mrema.





 Katika vurugu hizo dereva wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Haleluya Natai pamoja na wafuasi wa Chadema zaidi ya 15  walikamatwa na jeshi la polisi huku Nasari na aliyekua mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbles Lema wakitokomea kusikojulikana lakini kisha baadaye walionekana katika viunga vya kupigia kura.





Hatahivyo,katika hali isiyo ya kawaida naye mgombea wa Chadema katika kata hiyo,Prosper Msofe alionekana akirandaranda katika vituo vya kupigia kura huku akiwa na silaha yake aina ya bastola kiunoni hali ambayo ilizua mshangao kwa wapiga kura wa kata hiyo.





Katika vurugu hizo inadaiwa kuwa Nasari aliyekuwa akiongozana na lema wakiwa katika gari mojawapo walivamia ngome ya CCM iliyopo karibu na ofisi za chama hicho kata ya daraja mbili hali ambayo ilipelekea wafuasi wa CCM kuwavamia lakini Nasari alijiami na kisha kufyatua risasi tatu hewani.





Hatahivyo,kada wa CCM ,Kabwelwa Mturuka alijeruhiwa mkononi kwa kukatwa na panga na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema wakati wa majibishano karibu na kituo cha kupigia kura.





Katika  vurugu hizo mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arusha Martin Munis naye aliporwa simu yake ya mkononi na fedha ambapo  alitoa taarifa katika jeshi la polisi na kupewa AR/RB/13624/2012 ya shambulio la kudhuru mwili dhidi ya Nasari na Lema.





Wakati huohuo,wafuasi wa Chadema waliokuwa mita chache karibu na kituo cha kupigia kura cha sekondari ya Felix Mrema baada ya zoezi la uchaguzi kwisha, wakati wakisubiri matokeo, walivamia ofisi za CCM zilizokuwa karibu na kituo hicho na kisha kujaribu kung”oa bendera ya chama hicho lakini jitihada hizo zilizimwa na wafuasi wa CCM baada ya kumshusha kabla hajaikaribia bendera hiyo.





Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alipoulizwa juu ya matukio hayo alisema kwamba ni mapema sana kuzizungumzia lakini alikiri kushikiliwa kwa baadhi ya wafuasi wa CCM na Chadema ambao walihusika na vurugu katika uchaguzi huo.





Kwa upande wake,Nasari alipoulizwa juu ya hatua yake ya kurusha risasi hewani alipinga vikali lakini alipotafutwa Mwalusamba alikiri kurusha risasi hizo hewani huku akidai kwamba alifyatua kwa lengo la kujihami.
  Aidha saa nne usiku matokeo yamekemilika na kutangazwa na Modest Lupogo kwa niaba ya kaimu mkurugenzi wa jiji la Arusha Omary Mkombole ambapo alisema kuwa idadi ya watu walioandikishwa kupiga kura ni 16295 lakini waliojitokeza kupiga kura ni 3770 tu.

Akutangaza mshindi (diwani mpya wa kata ya daraja mbili)Lupogo alisema kuwa Prosper Msofe aliibuka kidedea kwa kura 2193  kupitia Chadema, akifuatiwa na mpinzani wake Philip Mushi Philip kupitia CCM aliyepata kura 1324, huku CUF ikipata kura 162, TLP wakipata kura 42, na NSSR kuambulia kura 22 

Wakati huo huo katika kata ya Bangata iliyoko wilayani Arumeru mkoani Arusha akitangaza matokeo hayo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha Halipha Idda alisema kuwa Olais Peter kupitia CCM ameibuka kidedea kwa kura 1177 na kuwaacha wapinzani wake Erick Samson Mollel kupitia Chadema kwa kura 881 huku Samweli Saimon  Ndosi kupiti TLP akiambulia kura 3 












0 comments:

Post a Comment