.

.
Wednesday, October 31, 2012

6:09 AM
Wachezaji wa Azam wakimbeba juu kocha wao Stewart Hall baada ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Jamhuri ya Pemba katika fainali iliyofanyika Januari 12 Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Picha na Jackson Odoyo.  

KOCHA Stewart Hall anatarajiwa kusaini mkataba mpya na timu ya Azam FC wakati wowote kuanzia sasa, hatua itakayomfanya kuingia kwenye orodha ya makocha wa klabu wanaolipwa vizuri barani Afrika.

Hall, raia wa Uingereza anatarajiwa kuwasili leo tayari kusaini mkataba mpya, akichukua nafasi ya Boris Bunjak aliyejiunga na Azam kuchukua nafasi ya Mwingereza huyo kabla naye kutimuliwa Jumatatu wiki hii.

Kutimuliwa Bunjak, raia wa Serbia kulikuja siku mbili tangu Azam kunyukwa 3-1 na Simba na kuporomoka kutoka nafasi ya pili ya msimamo Ligi Kuu mpaka ya nne.

Rais wa Sofapaka, Elly Kalekwa aliimbia Capital Sport kuwa, Azam wamemwomba radhi Hall na kumwahidi mkataba mnono ambao wameshindwa kumzuia.

"Sikupenda kuondoka kwake, lakini siwezi kumzuia. Azam wamempa mkataba unaofanya kuwa miongoni mwa makocha wanaolipwa zaidi Afrika."
"Kwanza walimwambia [Hall] wangependa kuendelea kuwa naye na kumwomba radhi kwa kufukuzwa kulikotokana na mapendekezo ya wachache," alisema rais huyo wa Sofapaka.

"Hall ni mweledi, tangu alipoingia mkataba na sisi. Azam walipomfuata alinipa taarifa na baada ya majadiliano tumekubali aende," Kalekwa alisema kwa huzuni.

Naye Bunjak alisema amepokea uamuzi huo kwa shingo upande na mshangao mkubwa hasa ukizingatia kuwa sababu ni matokeo ya kufungwa na Simba.

Bunjak alisema ameiongoza Azam kwa mafanikio kabla ya kucheza na Simba, akishinda mechi tano, sare tatu na kubaki nafasi ya pili kipindi kirefu.
Hata hivyo, Bunjak amesema anakubali hatua iliyochukuliwa dhidi yake, lakini akihoji vigezo vilivyotumika mpaka akafukuzwa.

ìHakuna timu isiyofungwa, kufungwa ni sehemu ya mchezo na ndiyo mpira wenyewe," alisema Bunjak.
"Haiingii akilini kama kigezo ni kufungwa na Simba. Inawezekana ni uamuzi tu uliokuwapo hasa kwa vile wanasema, "kocha anaajiriwa ili afukuzweî,î alisema Bunjak.

Alisema ni vigumu kumfukuza kocha kwa kufungwa mechi moja. "Ina maana timu hii (Azam FC) haitakiwa kufungwa hata mchezo?"

Bunjak alisema inashangaza kocha anatimuliwa kutoka timu iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo, tena ikiwa na mechi moja pungufu ya nyingine.

ìNimekubali, wamenilipa fedha zangu, sina jinsi kwa sasa nasubiri kurejea nyumbani Serbia siku mbili zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Bodi ya Azam, Hall atawasilileo kutoka Kenya na anatarajia kuanza kazi kesho katika mechi dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Chamazi.

0 comments:

Post a Comment