.

.
Friday, October 19, 2012

10:56 PM

chanzo cha habari gazeti la mwanaspoti
Wachezaji wa Simba wakipiga dua kwa Mungu, pamoja na kumuomba Mungu bado ushirikina wadaiwa kuwatafuna wachezaji wake
MICHAEL MOMBURI
BONGO kuna juju! Sikia hii inayomtokea staa mmoja mkubwa wa Simba.

Mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa amekuwa akitokewa na nyota mwenzake wa Simba kimiujiza nyakati za usiku, kisa ikiwa ni ugomvi wa kuwania namba uwanjani.

Amekwenda mbali zaidi na kudai kuwa alikuwa acheze mechi dhidi ya Kagera Sugar Jumatano wiki hii, lakini alimuomba kocha wake, Cirkovic Milovan amuondoe dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo kwa sababu ghafla alihisi mwili wake ukifa ganzi.

Kutokana na mambo mengi yanayomtokea straika huyo, rafiki yake ambaye pia ni mchezaji wa Simba amempeleka kimya kimya kwa mchungaji kufanyiwa maombi baada ya kuhisi kufanyiwa ushirikina katika kikosi hicho.

Tukio hilo lilitokea wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam baada ya mchezaji huyo (jina tunalo) kumwonea huruma rafiki yake kutokana na hali halisi na matukio aliyokuwa akimuhadithia kila mara.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa wachezaji hao wawili wa Simba (hawakutaka majina yao kutajwa hadharani), zinasema mchezaji anayedai kufanyiwa vitendo hivyo amekuwa akikumbana na mambo ya kutisha ndani na nje ya uwanja ikiwamo kufa ganzi miguu, kushindwa kuinua mguu kufanya uamuzi wa haraka na mambo mengine ya kukatisha tamaa, kubwa zaidi ikiwa ni kutokewa na mwenzake usiku.

Habari zinasema kuwa hata siku anavyoamka akiwa fiti, saa chache kabla ya mchezo hali hubadilika na kuanza kujihisi misuli inauma na hata katika mechi za hivi karibuni amewahi kumwomba kocha Cirkovic mara mbili asicheze ili kuepuka aibu uwanjani.

Mchezaji huyo aliyepiga stori na marafiki zake wa karibu wiki hii alifichua kuwa hali hiyo ilianza baada ya mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Azam.

Hali hiyo ilimfanya rafiki yake ambaye ni mchezaji wa Simba pia kumpeleka mwenzake kufanyiwa maombi kwa mchungaji mmoja maarufu jijini Dar es Salaam ili kupambana na nguvu hizo za giza ambazo anadai kufanyiwa na mwenzake kwa madai kuwa anamhofia kumpoka namba.

Mhusika licha ya kukiri kuwa hakuwahi kumwambia kiongozi yeyote wa Simba vioja anavyokumbana navyo kwa vile hakuwahi kuulizwa, alidai kuwa baada ya kwenda kwa mchungaji huyo na kufanyiwa maombi alimwona ndotoni ama kumtokea mara kadhaa mchezaji anayemfanyia vimbwanga pamoja na namba ya jezi yake.

"Namjua anataka kunimaliza lakini nitapambana naye kwa nguvu ya Mungu na atashindwa, mimi siamini kabisa mambo ya ushirikina lakini tangu (anamtaja jina) anipeleke kwa mchungaji mambo yangu yamekuwa tofauti kidogo.

"Hali ni ngumu sana, yaani hata nikigusa mpira saa nyingine mguu unakufa ganzi kabisa, naweza nikavua kiatu, lakini kukirudisha inakuwa tatizo. Sasa hiyo ni nini kama si uchawi?

"Lakini nitapambana na hili tatizo, lisipoisha tukienda mapumziko itabidi nifanye maombi sana," alisisitiza huku akikataa kutajwa gazetini.

Mchezaji huyo alimtaja mwenzake wa kikosi hicho ambaye anamfanyia vituko hivyo, lakini akaomba Mwanaspoti lisimuulize kwa sasa.

Kumekuwa na madai ya imani za kishirikina miongoni mwa wachezaji hususani wa klabu za Simba na Yanga sababu kubwa ikielezwa kuwa ni kuzidiana uwezo na wivu uwanjani.
 Chanzo cha habari na gazeti la mwanaspoti  

0 comments:

Post a Comment