.

.
Saturday, October 27, 2012

5:01 AM

CHAMA cha demokrasia na maendeleo(Chadema) ngazi ya taifa kimelazimika kuunda tume ya kuchunguza tuhuma  mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha za chama hicho mkoani Arusha sanjari na migogoro mbalimbali inayofukuta chini kwa chini  ndani ya chama hicho mkoani hapa.

 Baadhi ya wajumbe waliotajwa kuunda tume hiyo ni pamoja na wabunge wa Chadema akiwemo mbunge wa viti maalumu mkoani Kilimanjaro ,Grace Kiwhelu,mkurugenzi wa halmashauri na bunge,John Mrema sanjari na katibu wa mbunge wa Moshi mjini,Basil Lema.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyotufikia vimedai kwamba uamuzi wa kuunda tume hiyo umekuja baada ya uongozi wa Chadema ngazi ya taifa kupokea lawama mbalimbali kuhusu matumizi mabaya fedha za chama hicho zikiwemo zile za rambirambi za wahanga wa mauaji ya najuari 5 mwaka jana waliouwawa katika maandamano ya Chadema.

Itakumbukwa ya kwamba hivi karibuni tuliripoti habari za mjane,Asia Ismail ambaye marehemu mme wake aliuwawa katika maandamano ya januari 5 mwaka jana ambapo mjane huyo alikishutumu chama hicho kutafuna fedha za rambirambi zilichochangwa katika uwanja wa NMC huku akidai kwamba aliambulia zile zilizotolewa na kada maarufu wa CCM nchini,Mustafa Sabodo.

Vyanzo hivyo vya habari vimetuambia kuwa tume hiyo itawasili wiki hii mkoani Arusha kwa lengo la kuchunguza madai hayo ambapo itakutana na viongozi kadhaa wa Chadema  mkoani hapa wakiwemo makada mbalimbali.

Vyanzo hivyo vimesema kwamba tume hiyo pia itachunguza tuhuma za mbunge wa  zamani wa jimbo la Arusha mjini,Godbless Lema kudaiwa kuvuruga chama hicho mkoani hapa  ikiwa ni pamoja na kuingilia maamuzi mbalimbali yanayotolewa na  viongozi wa  chama hicho katika ngazi za wilaya na mkoa.

Hatahivyo,vyanzo hivyo vya habari vilienda mbali zaidi na kudai kwamba uamuzi wa kutuma tume hiyo mkoani hapa ulifuatia baada ya vigogo wa Chadema wakiwemo baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho  kutoridhishwa na hali  ya mwenendo wa chama hicho mkoani hapa huku wakidai kwamba endapo tuhuma hizo zikifumbiwa macho zitakipelekea chama hicho kupoteza mvuto mbele ya wanachama wake.

“Uamuzi wa kutuma tume hii ulitokana baada ya makao makuu kupokea tuhuma mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha za chama hapa Arusha na mifarakano ya chini kwa chini ndani ya Chadema mkoani hapa”kilisema chanzo cha habari

Mmoja wa wajumbe walioteuliwa  ndani ya tume hiyo(jina limehifadhiwa kwa sasa) amekaririwa akiwaambia baadhi ya wanachama wa Chadema mkoani Arusha kwamba hawakutarajia mkoa wa Arusha kama ungeingia  katika hali ya mtafaruku na kukabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Akihojiwa na waandishi wa habari, katibu wa Chadema mkoani Arusha,Aman Gorugwa alikanusha madai hayo na kusema kwamba hakuna tume inakuja Arusha kuchunguza tuhuma yoyote na viongozi waliotajwa wanakuja mkoani hapa kuongeza nguvu za kampeni katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Daraja mbili.

Alisisitiza kwamba huenda baadhi ya makada wa Chadema mkoani hapa wameamua kutumia jukwaa la viongozi wanaokuja mkoani hapa kuwapatia orodha ya tuhuma wanazotaka ziwafikie na kuwashangaa kwa kuwaita mamluki huku akihoji ni kwanini hawakuzifikisha mbele ya uongozi wa chama mkoani hapa.
 
 
Na Woinde Shizza

0 comments:

Post a Comment