Watoto wanaotoka katika mazingira magumu na kulelewa katika vituo maalumu, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaondoa watoto wenzao wanaoishi magerezani na mama zao bila hatia ,kwani licha ya kuteseka na hali mbaya ya mazingira iliyopo gerezani, wanakosa mahitaji ya msingi yanayomstahili mtoto kuyapata.

Aidha wamedai kuwa kitendo cha watoto hao kuendelea kuishi gerezani ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu na haki zingine wakati  hawana hatia yoyote hivyo wameililia serikali iwatoe na kuwakabidhi hata kwenye vituo vya kulelea watoto .

Watoto hao walitoa kilio hicho mbele ya mkuu wa mkoa wa Arusha ,Magesa Mulongo aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa madarasa mawili  katika kituo cha St.Gemma kilichopo kisongo jijini hapa, ambacho ni kituo pekee Tanzania kinacholea watoto waliopo gerezani ambao mama zao walifungwa.

Wakisoma risala yao kwa pamoja iliowasisimua wageni mbalimbali waliohudhulia hafla hiyo huku baadhi yao kujikuta wakibubujikwa na machozi akiwemo mkuu huyo wa mkoa,watoto hao wenye umri mdogo walisema kuwa kitendo cha wenzao kukaa gerezani kama wafungwa ni kuwanyima uhuru wa kuishi kwani hawana hatia wenye hatia ni wazazi ama walezi wao.

Waliendelea kusema ni vizuri serikali ikatafakari upya na kuona umuhimu wa kuwaondoa watoto hao waliopo magerezani  ili waungane na  wenzao waliopo uraiani na kuondokana na mateso wanayoyapata bila hatia ikiwemo kuathirika kisaikolojia kutokana na mazingira ya mageraza pamoja na  kukosa elimu.

‘’kwanini serikali inatufunga gerezani kwani tumekosa nini kama ni kosa wametenda wazazi wetu sisi tunafanya nini gerezani ,watoto wanashindwa kusoma ,kula vizuri na kucheza na wenzao, viongozi wa serikali tuoneeni huruma jamani, tunaomba wenzetu watolewe gerezani’’walisema.

Naye meneja wa kituo hicho,Flora Ndwata alisema  kuwa kituo hicho kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa na watoto watatu , hadi sasa kina jumla ya watoto 14 wenye umri wa miaka mitatu hadi 10 na kwamba kimeshindwa kuchukuwa watoto wengi kwa sababu ya kukosa fedha za kujiendeshea.

Alisema kituo hicho kilibuniwa na masister wa kanisa katoliki,shirika la St Gemme baada ya masister hao kuguswa na hali mbaya za watoto hao waliopo magerezani  na kuamua kuanzisha mkakati wa kuwasaidia kwa kuwaondoa kwa wazazi wao waliopo gerezani.

Alisema hatua hiyo iliwafanya wachangishane na kuamua kujenga vyumba viwili ambapo walifanikiwa kuwa na watoto wawili ambao walimudu kuwalea na baadae watu mbalimbali waliwaunga mkono kwa kuwasaidai michango iliyosaidia kuongezeka kwa watoto hao.

''tumekuwa tukiwauliza wamewapataje watoto hao wanasema wengine waliingia gerezani wakiwa na ujauzito na wengine walisema walipata ujauzito wakiwa huko na kujifungua''alisema Sister Flora

Aliongeza kuwa hadi sasa wana watoto kutoka gereza kuu la Isanga Dodoma,gereza la Babati na gereza kuu la Kisongo jijini hapa na kwamba wanatarajia kuomba watoto wengine kadri wanapo kuwa na uwezo wa kuwahudumia.

Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwanye harambee hiyo  ya kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa,alifanikiwa kuchangisha shilingi milioni 63.3 na kuvuka malengo ya shilingi milioni 46 zilizokuwa zikihitajika,huku ofisi yake ikichangia shilingi milioni 10.

 Wengine waliochangia ni pamoja na mkuu wa wilaya ya Arusha,John Mongela ambaye alichangia shilingi milioni 1pamoja na malori 9 ya mchanga na kokoto,kaimu mkurugenzi jiji la Arusha,Omari Mkombole shilingi milioni 10.3,Mkurugenzi Rich Hotel Joseph Masawe shilingi milioni 2.5.