.

.
Wednesday, October 31, 2012

12:43 PM
Watoto watano ,watatu wakiwa wa familia moja wamekufa Wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Ni baada ya kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono wakati walipokuwa wakichezea Bomu hilo lililookotwa kwenye vyuma chakavu na kudhani kuwa ni mpira.

Tukio hilo lilitokea Juma tano majira ya asubuhi huko Wilayani Karagwe mkoani Kagera Magharibi mwa Tanzania wakati watoto walipokuwa wakichezea kitu mfano wa mpira mdogo ,ambacho baadaye kilikuja kutambulika kuwa lilikuwa Bomu la kurushwa kwa mkono.
 Mkuu wa Wilaya wa Karagwe Bi Darli Rwegasira amesema kuwa watoto hao walilipukiwa na Bomu hilo ambapo watatu kati yao walikufa papo hapo huku wawili wakifia hospitalini.
Kwa Mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, awali mzazi wa watoto hao amekiri kuwa aliliona bomu nyumbani kwake hapo juzi ambapo watoto wake walikuja nalo baada ya kuliokota huku wakidhani kuwa ni mpira.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Philipo Kalangi alisema kuwa utafiti waliofanya umeonyesha kuwa Bomu hilo lililookotwa na kijana mmoja ambaye alikuwa akikusanya vyuma chakavu kwa lengo la kuviuza hapo wilayani karagwe.
Bomu hilo lilikuwa mojawapo katika vyuma alivyokuwa ameokota na baadaye watoto hao walienda kulichezea nyumbani kwao na hatimaye kusababisha maafa hayo.
Mkuu huyo wa Polisi mkoani Kagera alidokeza kuwa uchunguzi unaendelea ili kujua kwa undani Bomu hilo lilitokea wapi na iwapo kama kuna mabomu mengine yanayoweza kuwa yamebaki katika maeneo mbali mbali hapo Wilayani Karagwe.
Mkuu huyo wa Polisi hakuweza kukiri wala kukana moja kwa moja kuhusisha Bomu hilo Kama matokeo ya uwepo wa wakimbizi wa Rwanda waliowahi kuishi Wilayani hapo mwaka 1994 baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda ambapo Wilaya ya Karagwe ni moja ya wilaya zilizopokea wakimbizi wengi kutoka nchini Rwanda.
Uchunguzi zaidi unaendelea huku ukiwahusisha wataalam wa milipuko kutoka Polisi na jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

0 comments:

Post a Comment