.

.
Friday, October 19, 2012

6:22 AM

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, limedai kushangazwa kwake na ukimya wa serikali pamoja na vyombo vya dola kwa kutochukua hatua mapema za vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyokuwa vikitendeka.
Kanisa hilo pia limeeleza kusikitishwa kwake kwa vitendo vya uchomaji wa makanisa wakieleza kuwa kilichotokea Mbagala katika wiki ya kuadhimisha kifo cha Baba wa Taifa ni kebehi kwa watu waliokalia kiti chake.
Akizungumza katika ibada maalumu na kutoa salaamu za maaskofu wa kanisa hilo nchini kote kuhusiana na matukio ya kuchoma moto makanisa ya Kikristo, iliyofanyika katika kanisa la jimbo kuu Kusini Mbagala, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, alisema kuwa wamekutana kwa madhumuni ya kuonyesha majonzi yao kwa vitendo vya uvunjifu wa amani walivyoviita ni kuporomoka kwa umoja na mshikamano wa Watanzania.
Shao pia alisema kuwa madhumuni mengine ni kupokea matumaini ya Tanzania mpya katika msiba wa wenye dini na wasio na dini.
Aidha alisema kuwa katika ujio wa maaskofu 19 kutoka dayosisi mbalimbali za Tanzania hawakwenda Mbagala kuhukumu hata kama hawakubaliani na waliokashifu dini za wenzao.
Pia alisema kuwa hawakubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali kwa kisingizio cha kumtetea Mungu kwani kisasi cha dhambi wanamuachia Mungu aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.
Askofu Shao alifananisha kuwa kilichotokea Mbagala ni mateso ya kimbari ambayo mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema imezaa magugu yanayozaa matunda machungu.
Pia alilaani matumizi mabaya ya baadhi ya vyombo vya habari vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko ya kidini huku vikifumbiwa macho na vyombo vya dola.
“Uvumilivu wa dola hauna maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa letu na kwa Watanzania wote wawe wengi dhidi ya wachache au wachache dhidi ya wengi,” alisema.
Alihoji kuwa ni uvumilivu gani wakati wanashuhudia makanisa yakichomwa Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru na kwingineko? Wameshuhudia wizara zikivamiwa, vituo vya polisi vikichomwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishwa, viongozi waliostaafu wakizabwa makofu hadharani.
Shao alisema kuwa uvumilivu wa Wakristo umetafsiriwa kuwa unyonge na woga na kufafanua kuwa wanyonge na waoga hufika wakati wakasema basi pale wanapodhalilishwa kupita kiasi.
Naye Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, aliwataka Wakristo kuwa watulivu na kufunga na kuomba ikiwemo kuonyesha upendo.
Kanisa hilo ni miongoni mwa makanisa saba yaliyoteketezwa na waumini wa Kiislamu walioghadhabishwa na kitendo cha mtoto Emmanuel Josephat kukojolea kitabu chao kitakatifu cha Kuran.
Katika hatua nyingine kanisa la Faraja International Gospel, limechomwa moto na watu wasiofahamika na kusababisha hasara ya sh milioni 5.8.
Mchungaji wa kanisa hilo lililopo Yombo Makangarawe, Peter Kusaga, alisema kuwa watu hao walilivamia kanisa hilo majira ya saa 7 usiku kabla ya kuokolewa na majirani na wakati vifaa vya muziki vikiwa vimeteketea.
LHRC waonya
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeitaka serikali kuitisha mkutano wa dharura na viongozi wa dini zote ili kukomesha vitendo vinavyoendelea vya uvunjifu wa amani kwa kutumia imani za kidini.
Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, katika tamko lao kuhusu ghasia zilizotokea Mbagala kutokana na imani za dini na mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.
Kijo-Bisimba alisema katika mkutano huo, serikali inapaswa kushauriana na viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao kuwa na uvumilivu wa kidini ili wasije wakalifikisha taifa katika machafuko.
Aidha alitaka kukemewa kwa nguvu zote utumiaji wa propaganda ya udini katika siasa za ndani kwani inawagawa Watanzania na kuyumbisha demokrasia ya kweli.
“Hili suala la kuchanganya siasa na dini tumeshawahi kukemea katika ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2010 kwani tulishaona propaganda hizi za kidini zilitumika sana katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Hata hivyo hakuna jitihada zozote zilizofanywa kukomesha kuhusisha siasa na dini jambo ambalo ni hatari kama lisipofanyiwa kazi kwa mustakabali wa siasa ya vyama vingi nchini,” alisema.
Pia kituo hicho kimevitaka vyombo vya dola kuchukuwa hatua za tahadhari pale ambapo kuna mijadala ya wazi inayochochea chuki na kuhatarisha amani na utulivu wa nnchi.
Akigeukia mauaji ya Kamanda Liberatus Barlow, alisema walichokibaini ni kwamba jamii inaendeleza tabia ya kujichukulia sheria mikononi hali inayohatarisha amani na utulivu wa nchi.

0 comments:

Post a Comment