.

.
Tuesday, October 30, 2012

12:30 PM

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa S. Mulongo alipokuwa akielezea juu ya ziara ya Rais kwa waandishi wa habari
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya  siku tatu  katika jiji la Arusha kuanzia November 1 mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Stanslaus MuIongo Wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini mapema jana kwake.

Mulongo alisema kuwa ziara hiyo inaanza  rasmi  november moja ambapo ataanza kuzindua  hospitali ya Oluturmet iliyopo katika halmashauri ya arusha vijijini ambayo hapo awali ilikuwa ni kituo cha afya na sasa imepandishwa hadhi  na kuwa hospitali.

Aidha amefafanua kuwa siku hiyo ya kwanza pia ataweka jiwe la msingi katika barabara zinazojengwa jijini hapa ambazo mradi huo ni kwa hisani ya  benki ya dunia pamoja na serikali yaTanzania.

  Mulongo aliongeza kuwa baada ya hapo mheshimiwa rais atamalizia na uzinduzi wa nembo ya jiji la Arusha ambayo itazinduliwa rasmi katika makumbusho ya jiji ambapo uzinduzi huo itaambatana na sherehe za kusherehekea uzinduzi huo. 

mnara wa mwenge ni Moja ya alama iliyoko kwenye nembo  mpya ya jiji  likiwa katika ukarabati na kupakwa rangi kwa ajili ya sherehe za uzinduzi wa nembo ya jiji la Arusha

 Pia aliongeza kuwa siku hiyo hiyo rais atatumia fursa hiyo kuongea na wananchi wa jiji la Arusha katika uwanja wa kumbukumbu ya sheikh Amri Abeid.

 Mulongo pia alitoa wito kwa wananchi wa jiji la Arusha kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo wa jiji la arusha hususan pale ambapo Rais atakapo hutubia wananchi wa jiji la Arusha katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid .

Alisema novemba mbili Rais ataendelea na ziara yake katika taasisi ya Nalson Mandela ambapo atazindua rasmi taasisi hiyo  na baada ya hapo atatembelea kiwanda cha kutengenezea vyandarua  cha A to Z kuona shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho pamoja na kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na kuona namna ambavyo serikali itaweza kuwasaidia kuzitatua

Mulongo alisema kuwa siku ya tatu Rais anatarajia kwenda kufungua shule ya msingi ya Sokoine iliyopo ndani ya eneo la jeshi  la kulinda  taifa(JWTZ)  iliyopo wilayani Monduli  na baada ya hapo ataenda kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara kutoka Arusha hadi minjingu.

Awali Meya wa Jiji la Arusha Gaudence Lyimo alisema kuwa kupatikana kwa cheti hicho kunaipa mamlaka iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha nafasi ya kutumia rasmi hadhi ya Jiji.

Mea wa jiji la Arusha Mheshimiwa Gaudence Lyimo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo ofisini kwake juu ya uzinduzi wa nembo ya jiji.
Alisema Hii inawafanya kubadilisha kuanzia nyaraka zote za vitendea kazi pamoja na Nembo ya Manispaa ambapo sasa watatumia Nembo mpya.

Lyimo aliongeza kuwa Halmashauri hiyo ilianza tangu mwaka 1948 ikiwa ni Halmashauri ya Mji baada ya kukua kwa mji  ambapo ilibandishwa hadi na kuwa Manispaa mwaka 1980.

Kutokana na kupanuka kwa shughuli katika eneo la kilomita za mraba 93, Serikali iliamua kupandisha hadhi ya eneo hilo hadi kufikia kilomita za mraba 2,008.

Sanjari na hilo alisema kuwa hadhi hiyo ni kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 341 la Oktoba 14, mwaka 2011,”

         

0 comments:

Post a Comment