.

.
Monday, October 22, 2012

3:13 AM


WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amekabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), huku akitoa onyo kali kwa vigogo waliokwepa kuhojiwa na kamati kwa visingizio mbalimbali akisema ni lazima watahojiwa tu.
Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo yenye kurasa 285 na Mwenyekiti, Wakili Benard Mbakileki, na kuongeza kuwa kama suala analotaka kuhojiwa mhusika linahusu polisi, atapelekwa mbele ya jeshi hilo.
Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo baada ya Wakili Mbakileki kueleza kuwa baadhi ya watu muhimu TPA waliotakiwa kuhojiwa walikwepa kwa visingizio mbalimbali ikiwamo kuuguliwa, kufiwa na wengine kuzima simu kabisa.
Akijibu hoja hiyo, Dk. Mwakyembe alisema: “Kama walidhani kukwepa kamati ndio mambo yameisha, wanajidanganya. Watakuja kujibu mbele yangu na kama mambo yanahusu polisi tutawapeleka, hatutaacha mtu.”
Aliongeza kuwa kamati hiyo imefanya kazi ya kizalendo na kuahidi mambo yote iliyopendekeza watayafanyia kazi hatua kwa hatua, ili kuboresha bandari hiyo.
“Niwahakikishie hii kazi mliyoifanya haitakwenda bure, hadi kufikia Desemba mwaka huu, tutakuwa tumeyafanyia kazi mambo yote mliyopendekeza. Tutataka kuipa bandari sura mpya, kwa sasa inakosa ufanisi…tutakuja na uamuzi ambao hakitadokolewa kitu, kwani watakaodokoa, nao watadokolewa, kwani tusipofanya uamuzi huo hatutaikomboa nchi yetu,” alisema.
“Tulikuwa tunasikia habari za Twiga kusafirishwa kwenye ndege watu wakashangaa, lakini pale bandarini kontena na ukubwa wake linayeyuka. Mwaka juzi yaliyeyuka makontena 10, mwaka jana 26 na mwaka huu mawili na mambo yanatufanya tusiaminike,” alisema.
Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo, watafanya kazi kwa gharama yoyote, bila kumwonea mtu, ili kurekebisha bandari hiyo aliyoeleza kuwa iwapo ingesimamiwa vizuri nchi ingeweza kuendesha mambo mengi.
Aidha, alibainisha kuwa tangu kamati hiyo ilipoanza kufanya kazi, baadhi ya nchi jirani zimeanza kurejesha imani na bandari hiyo zilikemo Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Aliongeza kuwa iwapo baadhi ya watu wanakerwa na mabadiliko ndani ya TPA, waondoke kwani mjini kuna kazi nyingi za kufanya.
Pamoja na mambo mengine, Mwakyembe aliomba wapatiwe muda wa kuipitia ripoti hiyo kwa umakini na kwamba kila hatua watakuwa wakitoa taarifa kwa umma.
Kamati yanena
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbakileki, alisema katika kutekeleza uchunguzi waliwahoji watu 116 wakiwamo baadhi ya wajumbe wa Bodi na Wafanyakazi wa TPA pamoja na uongozi wa Vyama vya Wanyakazi (Dowuta), Mamlaka ya Mapato (TRA) Makao Makuu na kuonana na Kamishna Mkuu.
“Pia tulionana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) na maofisa wengine, eneo la Upakuaji na Upakiaji Mafuta (KOJ), Ticts na kuonana na Meneja Mkuu na maofisa wengine pia kujionea utendaji kazi.
“Polisi Chang’ombe tulikutana na Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke na maofisa wengine, kuzungumzia kukamatwa kwa magari yanayobeba mafuta machafu bandarini pamoja na jaribio la wizi wa kompyuta lililofanywa katika kituo cha WMA bandari kwa lengo ovu la kupoteza ushahidi,” alisema.
Alieleza kuwa wadau wengi walijitokeza bila kutarajia, wengi wao wakiwa na hamu ya kurudia mara mbili na pia mahojiano kwa mtu yalichukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa ambapo mtu mmoja alihojiwa kati ya dakika 50 hadi 180, hali iliyochangia mahojiano kufanyika hadi saa sita usiku.
Pia alieleza kuwa walipitia nyaraka mbalimbali zikiwemo sheria mbalimbali au Katiba ya nchi, Sheria ya TPA, sheria ya Mashirika ya Umma na mikataba mbalimbali.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Ramo Makani (Makamu Mwenyekiti), John Wanga, Halima Mamuya, Saidi Sauko, Richard Kasesela na Bernardina Mwijarabu.
Alisema katika utendaji wao kazi walisimamia nguzo moja kuwa ‘Ukweli na haki ndio utakaotuweka huru’ katika kulinda na kuendeleza rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Agosti 23, mwaka huu, Mwakyembe alitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, na viongozi wengine watatu, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazowakabili. Nafasi ya Mgawe kwa sasa inakaimiwa na Madeni Kipande kutoka Wizara ya Ujenzi.
Mbali ya Mgawe, vigogo wengine waliosimamishwa kazi ni wasaidizi wake wawili, Julius Mfuko na Hamad Koshuma pamoja na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Casian Nghamilo.
Baada ya kuwasimamisha viongozi hao, waziri huyo aliunda kamati hiyo na kuipa hoja 34 ambazo ziliundiwa hadidu za rejea tisa, ili kuchunguza chanzo cha kuzorota huduma TPA, hali inayochangia kukimbiwa na wateja wa ndani na nje ya nchi.
 CHANZO: TANZANIA DAIMA.

0 comments:

Post a Comment