.

.
Wednesday, October 17, 2012

7:44 AM

RAMBIRAMBI MSIBA WA WACHEZAJI RUSUMO FC
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya wachezaji watano wa timu ya Rusumo FC ya mkoani Kagera vilivyotokea jana jioni (Oktoba 16 mwaka huu).
 
Rusumo FC ilikuwa ikitoka kwenye mechi ya michuano ya Polisi Jamii Wilaya ya Ngara ambapo ikiwa njiani kurudi Rusumo kutoka mjini Ngara ilipata ajali ya gari na wachezaji watano kufariki papo hapo.
 
Wachezaji wengine ambao ni majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali zao zikiwa mbaya.
 
Msiba huo ni pigo kwa familia za marehemu, klabu ya Rusumo FC, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA) na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango wa wachezaji hao katika ustawi wa mchezo huu kupitia klabu yao.

TFF inatoa pole kwa familia za marehemu, Rusumo FC, NDFA na KRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Kutokana na msiba huo, mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacom zinazochezwa leo (Oktoba 17 mwaka huu) kutakuwa na dakika moja ya maombolezo ili kutoa heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amina
 
KIM KUSHUHUDIA MECHI ZA LIGI KUU Z’BAR
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen wikiendi hii ataanza ziara ya Zanzibar kuangalia Ligi Kuu ya Grand Malta kuwania ubingwa wa Zanzibar.
 
Kim anatarajia kushuhudia mechi zilizopungua tano akianzia kisiwani Pemba ambapo kati ya Oktoba 19 na 21 atashuhudiwa mechi mbili zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Gombani. Mechi hizo ni kati ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Grand Malta, Super Falcon ambao watacheza na vinara wa ligi hiyo Bandari, na baadaye mechi kati ya Duma na Bandari.
 
Baadaye atakwenda Unguja kwenye Uwanja wa Amaan ambapo baadhi ya mechi alizopanga kushuhudia ni kati ya Mtende na Chipukizi, Mundu na Jamhuri na KMKM dhidi ya Zimamoto.

0 comments:

Post a Comment