.

.
Friday, October 26, 2012

10:14 AM
Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Arusha vijijini, bi Mwantumu Dossi alipokuwa akiongea na BERTHA BLOG  ofisini kwake hivi karibuni
 Wanawake wametakiwa kusimama kutetea haki zao wenyewe pindi waonapo zinakiukwa kwa kufuatilia kwenye vyombo vya dola badala ya kukaa kimya pindi waonapo wanadhulumiwa.

Rai hiyo imetolewa na Afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Arusha vijijini, bi. Mwantumu Dosssi alipokuwa akiongea na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni.

Mwantumu alisema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakidhulumiwa haki zao lakini hukaa kimya hali inayowafanya kuteseka kulea familia    (watoto) peke yao na kusababisha baadhi ya watoto kushindwa kumudu maisha ya dhiki nyumbani na kukimbilia mtaani.

“Niwaombe wanawake tu kusimama wima kutetea haki zao pindi waonapo wanadhulumiwa kuliko kukaa kimya kusubiri mtu akutetee mbali na hilo pia  kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiujasiriamali kujipatia kipato cha kuwafanya kutokuwa tegemezi” alisema bi Mwantumu na kuongeza

“Endapo mwanamke ataweza kupigania haki yake au kujishughulisha na shughuli za kumuingizia kipato kitaweza kumsaidia kuendelea kulea familia yake pindi mumewe akiwa hayupo au amefariki lakini akibaki tegemezi atapata shida ya kulea familia na matokeo yake watoto huchoka maisha ya dhiki na kuamua kukimbilia mtaani na kuongeza idadi ya watoto wa mitaani” alisema Mwantumu.

Aliongeza kuwa mara nyingi wanandoa wanapoachana au mwanaume kufariki anayepata shida ya kulea familia ni mwanamke bila kuambulia chochote cha kumsaidia katika mzigo huo wa malezi peke yake ambapo wengi wao ni tegemezi wasiopenda kujishughulisha ambapo amefananisha utegemezi huo kama upumbavu kwa wanawake kudhika kuwa tegemezi badala ya kujishughulisha na hata biashara ndogo ndogo.

Akiongelea swala la watoto wa mitaani bi. Mwantumu alisema kuwa kwa sasa idadi ya watoto wa mitaani inazidi kuongezeka na sababu kubwa ni mifarakano ya familia na wengine wanatokana na hali ya uchumi (dhiki) wa majumbani mwao au wengine kuteseka kutokana na kuishi na watu baki(wasio wazazi wao)  hivyo sababu hizo humfanya mtoto kuona ni bora kutoroka nyumbani na kuingia mtaani kuomba omba.

Kutokana na hayo Mwantumu aliiomba jamii kuzingatia maadili, kanuni na taratibu ikiwemo kufuata mila na desturi za kitanzania kwa kuwasaidia watoto wasio na wazazi au kuwapokea na kuwalea watoto walioachwa na ndugu zao kwa kufa au kuugua kama wanavyowalea watoto wao.

Pamoja na bi. Mwantumu kusisitiza sana swala la wanawake kutokuwa tegemezi bali wajishughulishe na shughuli za kiujasiriamali pamoja na kujiunga na SACCOS mbali mbali, pia aliwataka wanafunzi walioko mashuleni kutokimbilia kuolewa bali wazingatie masomo ili kujimudu kimaisha hapo baadae.

0 comments:

Post a Comment