.

.
Wednesday, October 17, 2012

7:34 AM




Asha Maulid, Msichana mwenye umri wa miaka 20 na mkazi wa Kijiji cha Nduruma Wilaya ya Arumeru, anamlalamikia askari polisi mmoja, aliyefahamika kwa jina la Saidy Rashidi wa Kituo Kikuu cha Polisi Jijini kwa kumtelekeza baada ya kumzalisha.

Akizungumza Kituoni hapo Alhamis iliyopita, Asha aliwaambia Wandishi wa habari kwamba, alizaa na askari huyo mtoto wa kiume aitwaye Nasri Saidy ambaye sasa ana umri wa miezi nane  baada ya kuishi kama wapenzi na askari huyo katika makazi ya askari jijini hapa.

Msichana huyo aliendelea kudai mbele ya Wandishi wa Habari waliokuwa wamekusanyika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kufuatilia habari za kipolisi kwamba alitokea kupendana na askari huyo hatimaye kuishi naye katika nyumba za askari zilizoko maeneo ya kituo kikuu cha polisi ambapo baada ya miezi kadhaa askari huyo alimlazimisha kumzalia mtoto bila kufunga  naye ndoandoa.

“Baada ya miezi kadhaa ya kuishi naye akawa ananilazimisha kumzalia mtoto bila ndoa ambapo nikimuuliza alikuwa anasema kwa kuwa ananipenda hakuna shida tutaoana baada ya kuruhusiwa kuoa na mwajiri wake, kwani kwa sasa hawaruhusiwi kuoa kutokana na cheo chake, hivyo baada ya kuona kero za kuzaa zinazidi niliamua kubeba mimba ambapo ndipo hapo matatizo yalipoanzia”, alisema Asha.

Aliongeza: “Baada ya kubeba mimba na kufikia miezi 8 mwanaume akawa ananinyanyasa na kunipiga kila siku hadi kutokwa damu puani  hali iliyonisababisha kumwambia naenda kwetu”, alilalamika Asha na kuongeza:

“Baada aliniambia nichukue kila ninachoweza kuchukua na baada kuchukua alikuja nyumbani kwetu wakati sipo na kuvichukua na kwenda polisi kuandika maelezo kuwa mimi nimemvunjia nyumba na kumwibia vitu”, alidai Asha.

Asha alidai kwamba hali hiyo ilimsababishia wazazi wake kumchukia kutokana na askari huyo kuwadharau na kutumia uaskari wake kuwatishia ndugu zangu kuwa atawashtaki hali iliyowafanya ndugu hao kukosa amani.

Anasema kutokana na wazazi wake na ndugu wengine kumchukia alilazimika kuomba hifadhi kwa mama yake mdogo:

“Huko nilidhani nitapata ahueni kutokana na manyanyaso yake lakini huko ndiko nimekuwa nikiambulia kipigo kutoka kwa mwaname huyu na hatimaye kusababisha mama mdogo naye kunifukuza”, alieleza Asha kwa masikitiko huku akiwa amembeba mtoto wake Nasri ambaye alionekana na kuwa na siha njema na mchangamfu wakati wote.

Asha aliendelea kusema kuwa awali baada ya askari huyo kumfukuza nyumbani kwake alikuwa akimfuata siku moja moja kumtaka mumewe huyo kumpatia fedha za matumizi ya mtoto lakini alikuwa anaambulia matusi na kejeli kutoka kwa mumewe na pia wenzake walikuwa wakimshinikiza kumuweka ndani ya mahabusu ambapo aliwahi kulazwa  kituoni hapo bila kosa wala maelezo kwa madai kuwa amekuwa msumbufu.

Aidha alidai kuwa kutokana na mpenzi wake huyo kukataa kutoa fedha za malezi ya mtoto wao, aliamua kwenda kumshitaki Idara ya Ustawi wa Jamii, ambako anasema walimpa barua ya kumpelekea Mkuu wa Polisi Kituo cha Kikuu (OCS).

“OCS  alimwita mzazi mwenzangu huyo na kumkabidhi barua hiyo ya Ustawi wa Jamii ambapo  aliahidi kutoa matumizi ya mtoto lakini hadi sasa hakuna chochote anachotoa kwa ajili ya mtoto ambapo na zaidi ya hayo mwanzoni mwa Oktoba alikana kumtambua huyu mtoto wala na hata mimi mama yake”, alilalamika Asha kwa uchungu mkubwa.

Asha anasema kutokana na hali hiyo, naliomba Jeshi la Polisi kumsaidia kumsimamia askari huyo (mumewe) ili mtoto wake apate matunzo mazuri kwani ni haki ya mtoto huyo nay eye kupata matunzo kutoka kwa askari huyo.

Gazeti hili lilipowasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas, kuhusiana na madai ya msichana huyo, Kamanda huyo alitoa kauli tata.

Kwanza alisema azingeweza kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba hayo ni mambo binafsi lakini pia akasema kwamba kwa kuwa malalamiko hayo yanamhusisha askari wake atayafuatilia.

Kauli hizo tata za Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha zinafanya madai ya awali yaliyotolewa na Asha kwamba askari huyo amekuwa akitumia kivuli cha Jeshi la Polisi kumnyanyasa nay eye, mtoto wake, wazazi wake na familia yake kwa ujumla kuwa yanaweza kua na ukweli ndani yake.


0 comments:

Post a Comment