.

.
Monday, October 22, 2012

12:15 AM
CHAMA cha Alliance for Demokratic Change (ADC), kimewalipua Rais Jakaya Kikwete na mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, kwa madai kwamba wamehodhi rasilimali nyingi za taifa kwa maslahi yao binafsi na familia zao, kinyume cha taratibu na sheria za nchi.
Katika utawala wake, Mkapa aliweza kujimilikisha shamba kubwa la miwa la Mtibwa huko Morogoro pamoja na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, huku Rais Kikwete akituhumiwa kuhodhi rasilimali za madini.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Igoma jijini Mwanza juzi, Katibu Mkuu wa ADC, Lucas Limbu, alisema umaskini uliokithiri nchini unatokana na watawala kujali maslahi yao binafsi badala ya taifa.
Alisema kuwa kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kufumua mikataba ya kifisadi katika sekta ya madini ni kielelezo tosha kwamba na yeye ana maslahi katika mikataba hiyo.
“Watanzania tunalalamika mikataba ya madini ni mibovu. Lakini Rais Kikwete amekaa kimya. Hawa watu wamejipanga kunyonya rasilimali za taifa. Mkapa akiwa madarakani aliingiza marafiki zake Ikulu ili wanyonye nchi. Alijimilikisha mgodi wa Kiwira na shamba kubwa la miwa la Mtibwa. Kwa hiyo ADC inawaomba Watanzania waichukie na wainyime kura CCM mwaka 2015,” alisema.
Katika mkutano huo zaidi ya wanachama 200 walijiunga na chama hicho kwa kukabidhiwa kadi mpya, huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa wafuasi wa CHADEMA, waliokuwa wakiitikia ‘Power’ kila ilipotamkwa salamu ya ADC kwa kunyoosha vidole viwili vya alama ya ‘V’ juu.
Kwa upande mwingine, Limbu alimshukia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimtuhumu kushindwa kusimamia vema majukumu yake na kwamba kwa sasa hawezi kumsimamisha kazi mkuu wa wilaya wala mkoa.
Alisema Pinda ni muoga wa kuchukuwa hatua, huku akitolea mfano sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, aliposhindwa kumwajibisha bungeni baada ya kudaiwa kukusanya fedha kinyume na utaratibu.
Limbu alifafanua kuwa ADC ikiingia madarakani itahakikisha inasimamia na kuboresha zaidi sekta ya elimu na kuwa mradi wa kwanza wa serikali yake, kwani kwa sasa sekta hiyo imetelekezwa wakiwemo walimu.

Na Sitta Tuma-Mwanza

0 comments:

Post a Comment