.

.
Thursday, October 25, 2012

8:59 PM
Mhe. Christopher Ole Sendeka alipokuwa akiongea na waandishi na waandishi wa habari

MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara Christopher Ole Sendeka amesema watu wote ambao nyumba na mali zao zilikutwa na barabara ya Kia-Mirerani ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami watalipwa fidia.

Ole Sendeka aliyasema hayo juzi wakati akizindua kikundi cha wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite cha Tupendane Family kilichopo mji mdogo wa Mirerani ambapo zaidi ya sh6.2 milioni zilipatikana katika uzinduzi huo.

Alisema Serikali imeshatenga fedha za awali za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na miongoni mwa fedha hizo zitatumika kuwalipa fidia wote ambao barabara iliwakuta wameshajenga nyumba zao.

“Barabara imeshatengewa fedha za ujenzi wa awali na Waziri John Magufuli na nilipoomba ijengwe nilifikisha suala la fidia hadi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda hivyo hilo lisiwape wasiwasi,” alisema Ole Sendeka.

Akizungumza na wanachama wa kikundi cha Tupendane Family,mbunge huyo ambaye alisajiliwa rasmi kuwa mwanachama wa kikundi hicho alisema kikundi hicho kitaweza kuwainua kupitia Saccos au Vicoba.

Alisema kuwa kikundi hicho kina dhamira na malengo mazuri ya maendeleo kwa kujiinua kiuchumi,zaidi ya kusaidia wagonjwa au waliofiwa na kina sura ya kitaifa kutokana na kuwa na jamii ya makabila mbalimbali hapa nchini.

Naye,Katibu wa kikundi cha Tupendane Family Dickson Nakembetwa alisema kikundi chao kilianzishwa mwaka 2010 kikiwa na wanachama 30 na sasa kina wanachama 74 na wana akiba ya sh3 milioni kwenye benki ya NMB.

Nakembetwa alisema lengo la kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kusaidiana wakati wa matatizo na hadi hivi sasa wanakikundi saba wameshasaidiwa matatizo mbalimbali waliyonayo  kwa kutumia sh1.1 milioni.

Alisema kiingilio cha kikundi ni sh20,000 ada ya mwaka ni sh2,000 na hivi sasa wana mpango wa kutanua kikundi chao kwa kuanzisha biashara na wanahitaji sh200 milioni kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Na joseph lyimo-Manyara

0 comments:

Post a Comment