.

.
Tuesday, October 23, 2012

9:54 AM
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha, Halipha Idda(aliyesimama) alipokuwa akiahidi kufuatilia ubadhirifu wa fedha unaotuhumiwa kufanywa na wakuu wa idara, anayefuata ni mwenyekiti wa baraza hilo Saimon Saning'o(katikati) na kulia ni makamu mwenyekiti wa baraza hilo bi.Anna Agatha Msuya.

Madiwani la halmashasuri ya Arusha  wametishia kususia shughuli zote za maendeleo endapo mkurugenzi wa halmashauri hiyo halipha Idda hatawaonya na ikiwezekana kuwachukulia hatua kali za kisheria wakuu wa idara katika halmashauri hiyo kwa madai kuwa wanafanya shughuli zao huku wakikiuka sheria kanuni na Taratibu za nchi.

Madiwani hao wamesema hayo kwenye mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo ambapo wamesema kuwa wakuu wa idara mbalimbali hasa idara ya kilimo na fedha wamekuwa wakifanya kazi zao kinyume na taratibu hali inayohatarisha maendeleo ya halmashauri hiyo.

Walisema kuwa endapo mkurugenzi hatachukua hatua zozote hawako tayari kuumia kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache huku wananchi wakikosa imani na serikali yao kwa ajili ya baadhi ya watu wanaotanguliza matumbo yao na kuwafanyia madudu wananchi.

Walisema kuwa mara nyingi madiwani wamekuwa wakibuni miradi mbalimbali za kimaendeleo kwa wananchi wao lakini pindi ifikapo kwa mkuu wa idara hukataa endapo haina maslahi kwao hali inayorudisha nyuma maendeleo ya kata husika kwa wananchi wake kukata tamaa ambapo hali hiyo husababisha migogoro baina ya watumishi na wakuu hao kutokana na madiwani kutaka kulinda kura zao kwa kutetea miradi hiyo ikubalike.

Mbali na hilo pia waliwatuhumu idara ya fedha na kamati yake kwa kutowasilisha mahesabu ya uhakika kwani hesabu hizo hudhiirisha kila aina ya ubadhirifu  hali inayowafanya madiwani hao kumtaka mkurugenzi kufuatilia swal hilo kwa ukaribu.

Pia walisema kuwa mbali na ubadhirifu wa fedha pia ardhi imekuwa ikigawanywa bila utaratibu unaojulikana wala kuwepo kwa ripoti zake hali inayoonyesha manufaa hayo yanabaki mikononi mwa wahusika wa idara ya ardhi

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha Halipha Idda aliwaahidi madiwani hao kushughulikia swala hilo kwa kuwahoji watuhumiwa katika vikao vya ndani kuelezea hayo ambapo ikionekana ripoti zao zina kasoro au tuhuma hizo zina ukweli ndani yake atawachukulia hatua kali za kisheria wabadhirifu wa fedha za serikali.

Mbali na hilo pia aliwataka madiwani hao kuendelea kubuni miradi mbali mbali ya kuongeza pato la halmashauri kwa ajili ya maendeleo yao kwani wamekuwa wakitegemea fedha za serikali lakini zimekuwa zikichelewa sana na kukwamisha maendeleo ambapo alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuwahisha fedha za maendeleo kwani wamekwama kwa sehemu kubwa.
baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Arusha wakisikiliza kwa makini mmoja wao akiwasilisha hoja yake barazani hapo


0 comments:

Post a Comment