.

.
Tuesday, October 23, 2012

7:29 AM
MAKUNDI ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), yanaonekana kumwelemea Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, na sasa ameamua kutumia mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kukemea vitendo vya kudhalilishana na makundi wakati na baada ya uchaguzi.
Rais Kikwete pia alionya juu ya vitendo vya rushwa vinavyozidi kushamiri ndani ya chama hicho akisema kuwa visipochukuliwa hatua mapema, kuna hatari ya kukifikisha chama katika hatua mbaya.
Akifunga mkutano huo wa nane wa uchaguzi UWT, Rais aliwataka kufanya jitihada za kupunguza mgawanyiko uliotokea baada ya uchaguzi wao uliomalizika juzi.
Alisema imekuwa ni hulka sasa hasa baada ya kumalizika uchaguzi kwa wanachama kuendeleza na kuwekeana uhasama kama uliokuwepo wakati wa kampeni na wengine kuwaadhibu ambao hawakuwachagua hali ambayo ni mbaya sana kwa mustakabali wa chama.
“Ambaye hakukuchagua usimbague kwani hakushinda na sasa wewe ndiye kiongozi, hivyo una kila sababu ya kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitumikia jumuiya yake kwa ukamilifu.
“Itakuwa ni aibu sana na ajabu, pia utakuwa hujatenda haki kwa kumbagua ambaye hakukuchagua; natolea mfano kwangu katika uchaguzi uliopita, Prof. Mark Mwandosya hakushinda, lakini kwenye serikali yangu nilimuweka licha ya kuwa nilifanyiwa mambo ya ajabu sana ambayo ni vigumu kuyavumilia lakini kwa mwanasiasa, lazima uwe mkomavu,” alisisitiza.
Rais Kikwete aliwaasa wagombea wa nafasi mbalimbali wa UWT walioshindwa kutoweka visasi na walioshinda kutowapiga vijembe walioshindwa kwani kazi iliyo mbele ni kubwa kutokana na CCM hivi sasa kukabiliwa na hali ngumu ya ushindani wa kisiasa.
“Kweli tusipokemea vitendo hivi na kuviacha vikiendelea, tutakipeleka chama mahali pabaya, ninasikitika sana kusikia hata wanawake sasa wanajihusisha na utoaji rushwa ili kununua nafasi za uongozi kitu ambacho ni hatari sana,” alisema Kikwete.
Alifafanua kuwa chama kinakoelekea si kuzuri ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko.
Aliwapongeza wajumbe kwa kukamilisha uchaguzi wa viongozi watakaoongoza jumuia hiyo kwa muda wa miaka mitano na hata waliojitokeza kugombea kwani kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi.
Rais Kikwete aliongeza kuwa madhumuni ya CCM yaliyotamkwa katika katiba ni kushinda katika uchaguzi wa serikali kuu na mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda serikali kuu na serikali za mitaa.
Alisema ushindi wa CCM unapatikana kwa kukubaliwa na kuungwa mkono na wananchi wengi zaidi watakaojitokeza kupiga kura, hivyo kazi kubwa ambayo inatakiwa kufanywa na jumuiya za chama zilizoundwa ni kufanikisha hilo.
Kikwete alifafanua kuwa demokrasia ya uchaguzi ina athari zake kwani baada ya hapo kuna kazi kubwa ya kujenga umoja na mshikamano ili kuziba nyufa na mipasuko iliyotokea wakati wa uchaguzi.
Alisema kuwa huwezi kumchukia mwenzako kwa vile ameomba nafasi unayoitaka wewe, kwamba nafasi hiyo ni haki ya kila mwanachama, hivyo hakuna haja ya kuchukiana.
Rais Kikwete alifafanua kuwa uchaguzi una mifarakano mingi lakini kiongozi akishapatikana ni lazima aungwe mkono na kwamba wenye kuonyesha mfano ni wale walioshinda kwa kutowabeza walioshindwa.
Awali, Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba, alisema kuwa wamefanya mengi ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama na wamejipanga kuhakikisha wanaleta ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2015.
chanzo cha habari-Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment